• HABARI MPYA

  Wednesday, February 07, 2018

  SIMBA NA AZAM LEO NI VITA KUU YA UBINGWA LIGI KUU

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo sita kuchezwa kwenye viwanja tofauti nchini.
  Lakini macho na masikio ya wengi vitaelekezwa Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, ambako vinara Simba SC watawakaribisha Azam FC.
  Mchezo huo unatarajiwa kuteka hisia za wengi kwa sababu unawakutanisha farasi wawili wanaofukuzana kwenye mbio za ubingwa.
  Simba SC inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 38 na Azam FC ipo nafasi ya tatu kwa pointi zake 33, nyuma ya Yanga iliyo nafasi ya pili kwa pointi zake 34.  
  Hiyo ndiyo picha halisi ya upinzani wa mechi ya leo – kwani Azam FC anahitaji ushindi ili kupunguza gepu la pointi anazozidiwa na Simba, huku wapinzani wao hao nao wakihitaji ushindi ili kusogea mbele zaidi. 
  Katika mchezo wa leo, safu ya ushambuliaji ya Simba inatarajiwa kuendelea kuongozwa na Nahodha wake, John Raphael Bocco aliye katika msimu wake wa kwanza Msimbazi tangu awasili kutoka Azam FC Julai mwaka jana.
  Bocco yupo katika kiwango kizuri kwa sasa na amekuwa akifunga mfululizo katika mechi nne zilizopita nyumbani na ugenini, mambo ambayo anatarajiwa kuyaendeleza jioni ya leo pia.
  Lakini kinara wa mabao katika Ligi Kuu msimu huu, Emmanuel Okwi anatarajiwa kuwapo pia pamoja na viungi nyota kama Shiza Kichuya na Said Hamisi Ndemla.
  Usisahau wachezaji wengine watatu walisajiliwa pamoja na Bocco Julai mwaka jana kutoka Azam FC, kipa Aishi Manula na mabeki wanaoweza kucheza nafasi zote za nyuma hadi kiungo, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe ambao wanaongeza utamu wa mechi ya leo.
  Upande wa Azam FC bila shaka kipa Mghana, Razack Abalora ataendelea na majukumu yake ya langoni, akilindwa na mabeki mahiri kama Aggrey Morris na Mghana mwingine, Yakubu Mohammed.
  Beki wa pembeni anayepanda mno kusaidia mashmbulizi, Mzimbabwe Bruce Kangwa, kiungo Mcameroon, Stephan Kingue Mpondo, Nahodha HImid Mao na washambuliaji chipukizi, Shaaban Iddi Chilunda, Yahya Zayed, Iddi Kipagwile na Mbaraka Yussuph Abeid ndio tegemeo la Azam katika mchezo wa leo.
  Mshambuliaji mpya, Mghana Bernard Arthur naye anaweza kuwa na madhara pia akianzishwa jioni ya leo – na kwa ujumla mchezo wa leo unatarajiwa kuwa burudani nzuri kwa mashabiki.   
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbao FC na Singida United Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Mwadui FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Stand United na Lipuli FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Maji Maji na Tanzania Prisons Uwanja wa Maji Maji Songea na Ndanda FC na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
  Kesho kutakuwa na mchezo mmoja wa Ligi Kuu kati ya  wenyeji, Ruvu Shooting na Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA AZAM LEO NI VITA KUU YA UBINGWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top