• HABARI MPYA

  Thursday, February 08, 2018

  NGASSA AMALIZA UKAME WA MABAO WA ZAIDI YA MWAKA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa jana amefunga bao lake la kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya zaidi ya mwaka mmoja tangu arejee nchini kufuatia kwenda kucheza nje kwa muda. 
  Ngassa aliifungia Ndanda FC bao la kusawazisha jana dakika ya 63 katika sare ya 2-2 na timu yake ya zamani, Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kufuatia Eliud Ambokile kuwafungia wageni bao la kuongoza dakika ya 58.
  Ambokile akaifungia tena Mbeya City dakika ya 66, lakini Ndanda wakachomoa tena, safari hiyo Hemed Koja akifunga dakika ya 69 na mchezo umalazika kwa sare ya 0-0. 
  Mrisho Ngassa amecheza Mbeya City mwaka mzima bila kufunga bao

  Hili ni bao lake la kwanza Ngassa akiwa Ndanda na la kwake katika Ligi Kuu kwa ujumla tangu arejee kutoka Oman Desemba mwaka juzi na kujiunga na Mbeya City.
  Ngassa alikuwa Oman ambako alikuwa anachezea klabu ya Fanja aliyojiunga nayo Septemba 21, mwaka 2016 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea ya Free State Stars, alikoondoka Agosti mwaka huo baada ya kuomba mwenyewe kuvunja Mkataba kama ilivyokuwa Fanja.
  Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka 2015 akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.  Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (10) na Faria (8) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu.
  Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa alifanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka jana.
  Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.
  Ikumbukwe, Ngassa kisoka aliibukia Toto African ya Mwanza kabla kwenda Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba
  Mechi nyingine za Ligi Kuu jana, bao pekee la Mganda Emmanuel Okwi dakika ya 36 liliipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Taifa, wakati Singida United iliibamiza Mbao FC 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao yake yakifungwa na Shafiq Batambuze dakika ya 14 na Deus Kaseke dakika ya 58, huku Pastory Kiyombo akiwafungia wenteji dakika ya 50.
  Mwadui FC wakautumia vyema Uwanja wa nyumbani, Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga kwa kuibamiza 3-1 Mtibwa Sugar mabao yake yakifungwa na Evarigestus Mjwahuki dakika ya nne na 80 na Miraj Athumani dakika ya 69 na la wageni likafungwa na Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ dakika ya 20.
  Lipuli FC ikafanya maajabu, ikiwapiga wenyeji, Stand United 3-0 Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga, mabao ya Jamal Mnyate dakika za 12 na 54 na Adam Salamba dakika ya 18, wakati Maji Maji FC ikalazimishwa sare ya 0-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Maji Maji mjini Songea. 
  Ligi Kuu itaendelea leo kwa mchezo mmoja tu, wenyeji Ruvu Shooting wakiwaakribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA AMALIZA UKAME WA MABAO WA ZAIDI YA MWAKA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top