• HABARI MPYA

  Saturday, February 10, 2018

  MAHADHI AIPA USHINDI YANGA AKITOKEA BENCHI BAADA YA CHIRWA KUKOSA PENALTI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BAO la mtokea benchi Juma Mahadhi limeipa Yanga SC ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Saint Louis Suns United ya Shelisheli katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mahadhi aliye katika msimu wake wa pili Yanga SC tangu asajiliwe kutoka Coastal Union ya Tanga, alifunga bao hilo dakika ya 66 kwa shuti akimalizia kona iliyopigwa na winga Geoffrey Mwashiuya iliyozua kizazaa langoni mwa Saint Louis.
  Mahadhi alifunga bao hilo dakika moja baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib Migomba kama ilivyokuwa kwa mpishi wa bao lake, Mwashiuya ambaye naye alimbadili Emmanuel Martin.
  Juma Mahadhi akishangilia na kocha wake, George Lwandamina baada ya kuingia na kufunga bao pekee la ushindi leo 
  Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akienda chini baada ya kukwatuliwa na beki wa Saint Louis
  Pius Buswita wa Yanga akimtoka beki wa Saint Louis leo Uwanja wa Taifa  
  Kiungo Mkongo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi akiwa juu kuokoa kwsa kichwa dhidi ya mchezaji wa Saint Louis 
  Kiungo wa Yanga, Raphael Daudi akipambana na mchezaji wa Saint Louis leo

  Na ni bao ambalo lilikuja baada ya zaidi ya saa nzima ya Yanga kusota kujaribu kuupenya ukuta imara wa Saint Louis walioamua kucheza kwa kujihami muda wote ili kujaribu kutoruhusu nyavu zao kuguswa.
  Na Saint Louis wakawa wenye bahati zaidi baada ya Yanga kupoteza hadi nafasi ya kufunga kwa penalti mapema tu kipindi cha kwanza.
  Mshambuliaji Mzambia Obrey Chirwa alipiga nje mkwaju wa penalti dakika ya 25 baada ya beki wa Yanga, Hassan Ramadhani Kessy kuangushwa kwenye boksi na Herve Raktoarison ambaye alionywa kwa kwa kadi ya njano na refa Belay Tedesse Asserese.
  Kwa ujumla, Chirwa mshambuliaji tegemeo Yanga, leo alicheza nyuma ya bahati yake, kwani pamoja na kukosa penalti, alifanya makosa mara kwa mara na kupoteza nafasi zaidi za kufunga.
  Ikafikia Chirwa akapoteza hali ya kujiamini, lakini bado haikutosha kwa kocha Mzambia mwenzake, George Lwandamina kumpumzisha, pengine kutokana na ukweli kwamba hakuwa na mshambuliaji mwingine benchi kwa sababu timu inakabiliwa na maejruhi wengi.
  Pius Charles Buswita, tegemeo lingine la mabao Yanga pamoja na viungo wenzake, Ajib na Martin nao wote hawakuwa kwenye ubora wao leo na haikuwa ajabu walipotolewa kipindi cha pili.
  Nafasi nzuri zaidi ambayo waliipata wageni ni dakika ya 53 wakati Karl Hall kupiga nje akiwa anatazamana na lango la Yanga, baada ya kipa wa kukutana na mpira uliotemwa na kipa, Ramadhan Awa Kabwili.
  Baada ya ushindi mwembamba, Yanga watasafiri kwenda Victoria nchini Shelisheli kuyalinda matokeo hayo katika mchezo wa marudiano kati ya Februari 20 na 21, ili kusonga mbele.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Said Juma ‘Makapu’, Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita/ Yusuph Mhilu dk87, Raphael Daudi, Ibrahim Ajib/Juma Mahadhi dk65, Obrey Chirwa na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya.
  Saint Louis; Michael Ramandimius, Jean Paul Algae, Steve Henriette, Damien Maria, Betrand Esther, Travis Laurence, Herve Rakotoarison/ Yannick Julie dk60, Gervais Waye-Hive, Tahiry Andriamandimby na Elijah Tamboo na Karl Hall/ Mervin Mathiot dk62.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAHADHI AIPA USHINDI YANGA AKITOKEA BENCHI BAADA YA CHIRWA KUKOSA PENALTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top