• HABARI MPYA

  Tuesday, February 06, 2018

  CHIRWA APIGA HAT-TRICK YANGA YAIBAMIZA 4-0 NJOMBE MJI FC NA KURUDI NAFASI YA PILI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imerudi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji FC jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Pongezi ziende kwa mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyefunga mabao matatu peke yake, huku bao lingine likifungwa na mzawa, winga Emmanuel Martin.
  Kwa ushindi huo, timu ya kocha Mzambia, George Lwandamina inafikisha pointi 34 baada ya kucheza mechi 17 sasa ikizidiwa pointi nne tu na vinara Simba SC, ambao kesho watacheza mechi yao ya 17 dhidi ya Azam FC, iliyo nafasi ya tatu kwa pointi zake 33.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Hans Mabena wa Tanga, aliyesaidiwa na Khalifa Sika wa Pwani na Rashid Zango wa Iringa, mabao yote ya Yanga yalipatikana kipindi cha pili baada ya refa kukataa bao la mapema la kwanza la Chirwa. 
  Mfungaji wa mabao ya matatu ya Yanga leo, Obrey Chirwa (kushoto) akipongezwa na wenzake, Papy Kabamba Tshishimbi (katikati) na Pius Buswita (kulia) 
  Obrey Chirwa akipambana na beki wa Njombe Mji FC leo
  Mfungaji wa bao lingine la Yanga, Emmanuel Martin (kulia) akipiga mpira 
  Kipa wa Njombe Mji FC, Rajabu Mbululo akijaribu kuokoa kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu
  Beki wa Yanga, Gardiel Michael (kulia) akipiga krosi

  Chirwa alifunga bao la kwanza dakika ya 46 akimalizia pasi ya kiungo Pius Charles Buswita ambaye naye alipokea pasi ya kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi.
  Njombe Mji FC wakapatavpigo dakika ya 54 baada ya kipa wao, kipa wao, Rajabu Mbululo kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuudaka mpira uliokuwa unaelekea nyavuni nje ya eneo lake. Njombe walimtoa kiungo Claude Wigenge na kumuingiza kipa wa akiba, David Kissu.
  Kissu hakuweza kumzuia Chirwa kufunga bao lake la pili leo dakika ya 64 Chirwa anaifungia Yanga bao la pili kwa penati baada ya beki wa Njombe Mji, Ahmed Adewale kuunawa mpira kwenye boksi.
  Emmanuel Martin akaifungia Yanga bao la tatu dakika ya 68 akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuri la Juma Mahadhi.
  Na Chirwa akahitimisha shangwe za mabao za Yanga kwa kufunga bao la nne na la 10 kwake msimu huu dakika ya 86, akimalizia pasi nzuri ya Akilimali.
  Ligi Kuu itaendelea kesho; vinara Simba SC wakiwakaribisha Azam FC Uwanja wa Uhuru pia, Mbao FC na Singida United Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Mwadui FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Stand United na Lipuli FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Maji Maji na Tanzania Prisons Uwanja wa Maji Maji Songea na Ndanda FC na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
  Kesho kutakuwa na mchezo mmoja wa Ligi Kuu kati ya  wenyeji, Ruvu Shooting na Kagera Sugar Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani.
  Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Said Juma, Kelvin Yondan, Maka Edward, Raphael Daudi/Juma Mahadhi dk56, Papy Tshishimbi, Pius Buswita, Obrey Chirwa/Said Mussa dk87 na Emmanuel Martin/Buruan Akilimali dk84.
  Njombe Mji FC; Rajabu Mbululo, Agaton Mapunda, Harerimana Lewis, Ahmed Adewale, Laban Kambole, Aden Chepa, Willy Mgaya, Juma Mpakala, Ethienne Ngiladjoe, Ditram Nchimbi na Claude Wigenge/David Kissu dk56.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHIRWA APIGA HAT-TRICK YANGA YAIBAMIZA 4-0 NJOMBE MJI FC NA KURUDI NAFASI YA PILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top