• HABARI MPYA

  Friday, February 09, 2018

  AZAM FC KUIVAA KAGERA SUGAR BILA MANAHODHA WOTE JUMATATU KAITABA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kwa ndege mapema Jumapili kwenda Bukoba mkoani Kagera tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Jumatatu jioni Uwanja wa Kaitaba.
  Lakini Azam FC itaondoka bila wachezaji wake watano tegemeo, wakiwemo Manahoda wake wote wawili, Nahodha Mkuu kiungo Himid Mao Mkami na Msaidizi, beki Aggrey Morris Ambroce.
  Wakati Himid anasumbuliwa na maumivu ya goti, Aggrey atakosekana kwenye mchezo wa Jumatatu kwa sababu ya kadi tatu za njano.
  Aggrey Morris (katikati) atakosekana Jumatatu Uwanja wa Kaitaba kwa sababu ya kadi za njano
  Wachezaji wengine ambao watakosekana Jumatatu ni beki Mghana, Daniel Amoah anayesumbuliwa na maumivu ya goti pia, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye atabaki kwa ibada ya arobaini ya mama yake aliyefariki dunia mapema Januari na mshambuliaji Waziri Junior anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu.
  Msafara wa Azam FC utakaokuwa na kikosi cha wachezaji 19, utaongozwa na Mtendaji Mkuu, Abdul Mohammed.
  Azam FC inahitaji ushindi katika mchezo wa Jumatatu baada ya kupoteza mechi mbili dhidi ya wapinzani wake kwenye mbio za ubingwa, Simba (1-0) na Yanga (2-1) hivi karibuni hivyo kujikuta wanaangukia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
  Simba SC ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 41, wakifuatiwa na Yanga SC pointi 34, wakati Azam FC ina pointi 33 baada ya timu zote kucheza mechi 17.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC KUIVAA KAGERA SUGAR BILA MANAHODHA WOTE JUMATATU KAITABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top