• HABARI MPYA

    Sunday, February 04, 2018

    AMBAVYO JOHN BOCCO NI MFANO WA KUIGWA MBELE YA SURA MBILI ZA MASHABIKI

    MASHABIKI wa Simba jioni ya leo wameimba jina ‘Bocco’ kwa furaha wakati na baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani ambao timu yao iliibuka na ushindi wa mabao 3-0  Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Hiyo ni kutokana na Nahodha wao huyo kufunga mabao mawili katika ushindi wa leo na kuendelea kujipambanua kama tegemeo la mabao la timu katika kampeni za ubingwa wa kwanza baada ya miaka mitano.
    Ushindi huo unaifanya Simba ifikishe pointi 38 baada ya kucheza mechi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tano zaidi ya Azam FC wanaoshika nafasi ya pili huku pia wakiwazidi pointi saba mabingwa watetezi, Yanga SC walio nafasi ya tatu,
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hans Mabena wa Tanga aliyesaidiwa na Arnold Bugando wa Singida na Slyvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na Bocco dakika ya 22 akitumia vizuri urefu wake kutumbukiza mpira nyavuni kwa kichwa baada ya kona ya winga Shiza Ramadhani Kichuya kutoka upande wa kulia. 
    Hapo ndipo shangwe za; “Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco,” zilipoanza kurindima Uwanja wa Uhuru sambamba na makofi ya pongezi.
    Simba SC iliongeza kasi ya mashambulizi langoni mwa Ruvu Shooting kusaka mabao zaidi, lakini ikaishia kukosa mabao ya wazi na almanusra Bocco afunge bao lingine dakika ya 44 kama si mpira aliopiga kwa kichwa tena kumalizia krosi ya beki wa kulia, Shomary Kapombe kwenda nje sentimita chache.
    Ruvu ikapata pigo dakika ya 45, baada ya beki wake, Mau Bofu kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Arnold Okwi aliyeshindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Mrundi, Laudit Mavugo.
    Kipindi cha pili, Simba ya kocha Mfaransa Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma ilikianza na mabadiliko, ikipumzisha kiungo chipukizi Said Hamisi Ndemla na kumuingiza mkongwe Mwinyi Kazimoto Mwitula na Ruvu Shooting ya kocha Mzanzibari Abdulmatik Haji anayesaidiwa na mzalendo mwenzake, Suleiman Kidungwe ilimuingiza Yussuph Nguya kuchukua nafasi ya Issa Kandulu.
    Mabadiliko hayo hayo yaliinufaisha Simba SC na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi, Bocco akifunga bao lake la tisa la msimu katika Ligi Kuu sasa anazidiwa matatu tu na, Okwi  anayeongoza kwa mabao yake 12. 
    Lakini ni kiungo Muzamil Yassin aliyefunga bao la pili dakika ya 66 akimalizia krosi nzuri ya winga Shiza Kichuya waliyesajiliwa pamoja Simba SC msimu uliopita kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro,
    Bocco aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC tangu asajiliwe kutoka Azam FC Julai mwaka jana akakamilisha shangwe za mabao za Simba leo kwa kufunga bao la tatu dakika ya 75 akitumia vizuri makosa ya kipa Abdallah Rashid kutoka bila mahesabu.
    Ruvu Shooting wakapata pigo lingine dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika za kawaida za mchezo, kufuatia mchezaji wake, Adam Ibrahim kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Kichuya.
    Na baada ya mchezo, shangwe za “Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco, Bocco,” ziliendelea, tena kwa nguvu zaidi ndani nan je ya Uwanja.
    Mashabiki waliokuwa wanaimba “Bocco, Bocco”, leo ndio wale wale ambao siku za mwanzoni walikuwa wanamzomea mshambuliaji huyo na kumlaumu pia aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Marius Omog kumpanga.
    “Toa huyoo, Toa huyoo, Toa huyoo,” ni kelele ambazo alikuwa anapigiwa Bocco katika siku za mwanzo za maisha yake Simba SC, lakini leo mambo yamebadilika na tayari kijana huyo ni kipenzi cha wana Msimbazi.
    Hakuna kingine zaidi ya kazi yake nzuri uwanjani kwa sasa, akifunga mabao mfululizo na kuisaidia Simba kukaa kileleni mwa Ligi Kuu ndivyo vimemfanya awe kipenzi cha wapenzi wa timu kwa sasa.
    Lakini hiyo imetokana na uvimilivu wake kama mchezaji, kuziba masikio wakati wa kelele za “Toa huyoo” na kuongeza bidii ya mazoezi ili awe fiti na kufikia kukonga nyoyo za mashabiki wa Msimbazi.
    Akiwa na beji ya Unahodha wa timu aliyopewa kwa hekima za kocha Msaidizi, Mrundi Masoud Juma, Bocco anaanza kufurahia maisha ya kazi Simba – lakini haiondoi ukweli kwamba amejifunza kuhusu sura mbili za mashabiki.
    Bocco sasa anajua shabiki si adui, wala rafiki wa kudumu. Shabiki ni rafiki yako pale tu unapokuwa katika kiwango kizuri na kufanya kile anachokipenda. Lakini unapokuwa katika kiwango duni na huna msaada kwa timu, shabiki hawezi kuwa rafiki yako.
    Lakini kwa kuwa soka ipo kwa ajili ya wapenzi na mashabiki wake, ambao ndio wapenzi na mashabiki wa timu, mchezaji anatakiwa kuwaheshimu watu hao siku zote na wakati wote.
    Barani Ulaya, mchezaji anayethubutu kumdhuru shabiki anachukuliwa hatua kali mfano Novemba mwaka jana, beki wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Patrice Evra alifungiwa miezi saba na Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) kabla ya kuvunjiwa mkataba na klabu yake, Marseille baada ya kumpiga teke shabiki wa klabu hiyo kabla ya mechi ya Europa League dhidi ya Vitoria wiki iliyotangulia. 
    Wachezaji Ulaya wanalipwa Pauni hadi 600,000 kwa wiki mgano Alexis Sanchez pale Manmchester United, lakini wote wanajua bosi wao ni shabiki anayelipwa kiingilio chake kutazama mechi na hata kununua jezi zenye jina la mchezaji.
    Hupaswi kuwachukia mashabiki hata wakikuzomea. Hata wakifanya nini, kwa sababu mwisho wa siku hao ndio wanachangishana fedha kwa staili ya viingilio na zinasaidia uendeshwaji wa klabu na mchezo kwa ujumla.
    Na hapa ndipo unapoweza kumuinu John Raphael Bocco na kumuweka mbele kama mchezaji mfano wa kuigwa, aliyestahmili kuzomewa na sasa anaimbwa kishujaa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMBAVYO JOHN BOCCO NI MFANO WA KUIGWA MBELE YA SURA MBILI ZA MASHABIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top