• HABARI MPYA

  Friday, February 09, 2018

  AJIB, ROSTAND WAREJEA MAZOEZINI YANGA IKIJIANDAA KUWAVAA ST LOUIS KESHO LIGI YA MABINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DARR ES SALAAM
  MCHEZAJI kipenzi cha wana Yanga, Ibrahim Ajib Migomba jana amefanya mazoezi kikamilifu kuelekea mechi ya kwanza wa Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Saint Louis FC ya Shelisheli kesho Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na Ajib aliye katika msimu wake wa kwanza tangu asajiliwe kutoka Simba, idadi ya majeruhi Yanga imeanza kupungua taratibu, baada ya wengine watatu, kipa Mcameroon Youthe Rostand, beki mzawa Juma Abdul na kiungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko kufanya pia mazoezi kikamilifu jana.
  Benchi la Ufundi la Yanga chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina linatarajiwa kuendelea kuangalia hali za wachezaji hao katika mazoezi ya leo Uwanja wa Gymkhana kuelekea mechi ya kwanza wa Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Saint Louis FC ya Shelisheli kesho.
  Kipenzi cha wana Yanga, Ibrahim Ajib jana amefanya mazoezi kikamilifu kuelekea mechi na Saint Louis FC kesho  

  Aidha, mabeki wazawa Pato Ngonyani na Andrew Vincent ‘Dante’ nao wameanza mazoezi mepesi peke yao, kuashiria wanaweza kurudi kwa ajili ya mchezo wa marudiano wiki mbili baadaye.
  Majeruhi wengine Yanga ni mabeki Mwinyi Hajji Mngwali, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na washambuliaji Yohana Oscar Nkomola, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
  Ikumbukwe jana Yanga ilizuiwa kufanya mazoezi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na kulazimika kwenda Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi Tanzania, kilichopo Kurasini.
  Uongozi wa Uwanja wa Taifa umesema kwa kuwa nyasi za Uwanja huo zimeoteshwa hivi karibuni, bado haziwezi kuhimili mikiki mfululizo ya mechi.
  Kwa sababu hiyo zaidi ya mechi hizo za kwanza za Raundi ya Kwanza ya michuano ya Afrika Jumamosi na Jumapili ni wageni tu, Saint Louis FC na Gendarmerie Tnale wataruhusiwa kufanya mazoezi Ijumaa na Jumamosi.
  Saint Louis FC watafanya mazoezi leo jioni wakati Gendarmerie Tnale wanaweza kufanya Jumamosi asubuhi au mchana na kuna uwezekano pia Simba SC wakaruhusiwa kufanya mazoesi usiku wa Jumamosi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AJIB, ROSTAND WAREJEA MAZOEZINI YANGA IKIJIANDAA KUWAVAA ST LOUIS KESHO LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top