• HABARI MPYA

  Thursday, January 04, 2018

  YANGA SC YAENDELEZA UMWAMBA KOMBE LA MAPINDUZI, YAIPIGA JKU 1-0…ASANTE KESSY

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  BAO la dakika ya 90 la beki Hassan Ramadhani Kessy limeipa ushindi wa 1-0 Yanga SC dhidi ya JKU katika mchezo wa Kundi B Kombe la Mapinduzi jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Sifa zimuendee mwenyewe Kessy kwa bao hilo, kwani aliingia na mpira ndani kwa kasi kutokea pembeni akampasia Pius Buswita aliyemsogezea mbele beki huyo kwa pasi ya kisigino akaikuta na kufunga.
  Kwa ushindi huo mwembamba, Yanga SC inafikisha pointi sita baada ya mechi mbili, ikiwemo ya kwanza waliyoshinda 2-1 dhidi ya Mlandege juzi.  
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Nassor Salum aliyesaidiwa na Iddi Khamis na Mussa Hemed ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza timu zote zilifanya mabadiliko.
  JKU walianza kumtoa Ali Omar na kumuingiza Said Zege dakika ya 38, kabla ya Yanga kumpumzisha mshambuliaji Matheo Anthony na kumuingiza Yohanna Oscar Nkomola.
  Katika kipindi hicho ilishuhudiwa JKU wakitawala mchezo na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Yanga, lakini hayakuwa na madhara.
  Kwa Yanga, Matheo Anthony alipoteza nafasi mbili nzuri kabla ya kutolewa, zote akipiga juu ya lango akiwa amebaki anatazamana na kipa baada ya kuwatoka walinzi. 
  Kipindi cha pili, Yanga walikianza na mabadiliko wakiwapumzisha beki na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Juma Mahadhi na kuwaingiza viungo Raphael Daudi na Said ‘Ronaldo’ Mussa.
  Kiungo Said Juma ‘Makapu’ alirudi kucheza pamoja na Kevin Yondan beki ya kati kuziba nafasi ya Cannavaro na Raphael Daudi akasogea nafasi ya kiungo, huku Said Ronaldo akiongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.
  Bado JKU wakiongozwa na kiungo mdogo wa umri na umbo mwenye uwezo mkubwa, Feisal Salum ‘Fei Toto’, waliendelea kutawala mchezo hadi Yanga ilipofanya mabadiliko mengine, ikiwaingiza Geoffrey Mwashiuya na Ibrahim Ajib kuchukua nafasi za Papy Kabamba Tshishimbi na Emmanuel Martin.
  Kwa mabadiliko hayo, Yanga nao wakaanza kuwainua mashabiki wao kwa shangwe kutokana na mchezo mzuri na mashambulizi ya kusisimua hadi kupata bao pekee dakika ya 90, shujaa beki waliyemtoa kwa mahasimu wao, Simba mwaka juzi, Kessy.
  Mchezo uliotangulia wa kiporo kati ya Taifa Jan’gombe na Singida United uliochezwa kwa dakika 45 ulimalizika kwa sare ya 0-0.
  Maana yake Singida United inaibuka na ushindi wa 3-1 mabao iliyovuna katika mechi ya jana iliyochezwa kwa dakika 45 tu kabla ya kuvunjika kwa sababu ya mvua kubwa iliyonyesha jana.
  Kikosi cha JKU kilikuwa; Hajji Juma, Hafidh Mohammed, Edward Mayunga, Issa Dau, Khamis Ali, Feisal Salum, Mbarouk Fakhi/Said Salum dk82, Isihaka Omar, Nassor Juma/Salum Mussa dk53, Ali Omar/Said Zege dk38 na Mohammed Mpopo.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Raphael Daudi dk46, Said Juma ‘Makapu’, Pius Buswita, Papy Kabamba Tshishimbi/Geoffrey Mwashiuya dk76, Juma Mahadhi/Said ‘Ronaldo’ Mussa dk46, Matheo Anthony/Yohanna Nkomola dk41 na Emmanuel Martin/Ibrahim Ajib dk58.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YAENDELEZA UMWAMBA KOMBE LA MAPINDUZI, YAIPIGA JKU 1-0…ASANTE KESSY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top