• HABARI MPYA

    Wednesday, January 10, 2018

    URA YAITUPA YANGA NJE KWA MATUTA KOMBE LA MAPINDUZI

    Na Salum Vuai, ZANZIBAR
    YANGA SC itapanda boti kurejea mjini Dar es Salaam kesho baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapunduzi kwa penalti 5-4 na URA ya Uganda kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Yanga SC imeendeleza utamaduni wake wa kufanya vibaya kwenye hatua ya matuta baada ya mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa kumdakisha mpira kipa wa URA, Alionzi Nafian.
    Chirwa alikosa penalti ya mwisho ya Yanga baada ya wenzake wote wanne, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na wazalendo Hassan Ramadhani Kessy, Raphael Daudi Lothi na Gardiel Michael Mbaga kufunga.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Issa Hajji, aliyesaidiwa na Shehe Suleiman na Mwanahija Makame, penalti za URA zilifungwa na Patrick Mbowa, Enock Kigumba, Shafiq Kagimu, Jimmy Kulaba na Brian Majwega.
    Katika dakika 90 za mchezo timu zote zilishambuliana kwa zamu, ingawa URA ndiyo walioonekana kulitia misukosuko zaidi lango la Yanga.
    Tofauti na ilivyotarajiwa kwamba kuingia kwa Chirwa kipindi cha pili kwenda kuchukua nafasi ya Pius Buswita kungeiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya Yanga, lakini Mzambia huyo alishindwa kucheza vizuri kutokana na kile kilichoonekana wazi hakuwa fiti.
    Chirwa alikuwa kwao Zambia kufuatia mgomo wake wa kushinikiza alipwe fedha za usajili na amerejea juzi Dar es Salaam na moja kwa moja kusafirishwa kuletwa Zanzibar kabla ya kuingizwa uwanjani kipindi cha pili.   
    Na hata penalti aliyokwenda kupiga ilikuwa ya ovyo kabisa na kipa wa URA hakuhitaji kujisumbua kuiokoa, kwani mpira ulimkuta mikononi tena pale pale aliposimama. 
    Nusu Fainali ya pili inafuatia kati Azam FC na Singida United Saa 2:15 usiku hapo hapo Uwanja wa Amaan na Fainali itachezwa Jumamosi.
    Kikosi cha URA kilikuwa; Alionzi Nafian, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allan Munaaba, Patrick Mbowa/Jimmy Kulaba dk92, Julius Mutyaba, Nicholas Kagaba, Shafiq Kagimu, Bokota Labama/Peter Lwasa dk70, Kalama Deboss na Charles Ssempa/Hudu Mbulikyi dk70.
    Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent, Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita/Obrey Chirwa dk53, Said Juma ‘Makapu’/Raphael Daudi dk92, Ibrahim Ajib, Juma Mahadhi/Yohann Nkomola dk75 na Emmanuel Martin/Gardiel Michael dk85.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: URA YAITUPA YANGA NJE KWA MATUTA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top