• HABARI MPYA

    Wednesday, January 03, 2018

    TFF YATAJA HATUA ILIZOCHUKUA JUU YA MECHI ZA DARAJA LA KWANZA ZILIZOLALAMIKIWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemuagiza Kaimu Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidau kufuatilia kwa kina tuhuma za uonevu katika michezo ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania baina ya Dodoma FC na Alliance ya Mwanza mjini Dodoma na kati ya Pamba ya Mwanza na Biashara mjini Musoma.
    Hiyo inafuatia Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutoa taarifa ya kushtushwa na kusikitishwa na malalamiko ya wadau wa soka nchini kuhusu vitendo vya uonevu na upendeleo vinavyodaiwa kujitokeza katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza.
    Rais wa TFF, Wallace Karia (kushoto) na Makamu wake, Michael Wambura (kulia)

    Karia amesema kwamba hatua za awali alizochukuwa Kaimu Katibu Mkuu ni pamoja na kuwasiliana na Kamishna wa mchezo na msimamizi wa Kituo cha Dodoma ambao wote walimpatia maelezo ya kilichotokea na baada ya hapo Kaimu Katibu Mkuu akawasiliana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi chombo kilichopewa dhamana ya kusimamia Ligi zote kubwa nchini ikiwemo Ligi Daraja la Kwanza, Afisa Mtendaji Mkuu naye alieleza Taarifa aliyopewa na Afisa wa Bodi aliyekuwa Dodoma. 
    “Kwanza TFF inapenda kumpongeza Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa michezo ikiwemo Mpira wa Miguu. Baada ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL)  Dodoma FC vs Alliance na Biashara vs Pamba kuliibuka malalamiko mengi ambayo yaliwafikia viongozi wakuu wa TFF na kuyatolea tamko,”. 
    Kaimu Katibu Mkuu baada ya kuwasiliana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi alikuwa na mawasiliano yaliyochukuwa muda mrefu na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Ndugu Mohamed Kiganja ili kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kujiridhisha na jambo lililojitokeza.
    Aidha, Kaimu Katibu Mkuu amekuwa na mawasiliano na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Yusuph Singo kuhusiana na suala hilo mara baada ya michezo ile kumalizika na wamekuwa na ushirikiano mkubwa katika kulifuatilia jambo hilo kwa karibu.
    Baada ya kupata taarifa mbalimbali Kaimu Katibu Mkuu alipeleka taarifa kwa Rais wa TFF ambaye aliagiza Kikao cha Kamati ya saa 72 kikae haraka iwezekanavyo ambapo Bodi ya Ligi walikuwa wanasubiri ripoti ambayo kwa mujibu wa kanuni za Ligi ni saa 48 na tayari taarifa zote zimefika jana kikao kimepangwa kufanyika kesho. 
    Rais, Karia bado aliona haitoshi hata kabla Waziri Mwakyembe "hajazungumza na Waandishi wa Habari" aliita Wana Habari na kati ya alivyozungumza ni kuhusu kinachoendelea Ligi Daraja la Kwanza na alionesha dhamira ya kuwashughulikia wote wanaotaka kuharibu Ligi zetu kwa Upana wake na kwa Ligi zote VPL, FDL na SDL na hasa kwa Michezo inayohusisha timu za Makundi yote zilizo katika nafasi ya kupanda au kushuka Daraja (FDL na SDL)  kuanzia mechi zinazolalamikiwa na kuhakiki za aina hiyo zisizolalamikiwa,lakini pia katoa maagizo kwa Kaimu Katibu Mkuu kuwaandikia barua TAKUKURU ili wachunguze matukio yote hayo yaliyojitokeza na yanayoendelea na TFF ipo tayari kutoa Ushirikiano wa kutosha katika Uchunguzi huo.
    “TFF inapenda kusisitiza kuwa viongozi wake wakuu hawajihusishi na jambo lolote lile la kupendelea mikoa wanayotoka ndiyo maana wakati Ndugu Wallace Karia alipokuwa Makamu wa Rais wa TFF timu tatu za Tanga Coast Union, African Sports na Mgambo zilishuka kwa mpigo,”. 
    “Katika mfumo wa kitaasisi unaoendesha TFF wenye jukumu la kusimamia Ligi zetu ni Bodi ya ligi, ambao ndiyo wasimamizi wa moja kwa moja wa ligi daraja la kwanza hivyo maamuzi hufanywa kwa kutumia vyombo vya kitaasisi na hakuna nafasi kwa Rais wa TFF au Makamu wake kuingilia vyombo vya TFF ambavyo vinafanya kazi ya kusimamia ligi,”. 
    “TFF inawajibika kama msimamizi mkuu wa Soka nchini kuhakikisha vyombo vyake vinatenda haki kikiwemo chombo chake kinachosimamia ligi zetu TPLB,”. 
    “TFF pia kwa maelekezo ya Rais Karia kwa Kaimu Katibu Mkuu, ameelekeza kuangaliwa upya na Kufanyiwa marekebisho ya TIJA kwa Ratiba ya WAAMUZI (kama itabainika haja ya kufanya hivyo) kwa Michezo yote ya FDL inayokutanisha TIMU zenye nafasi ya kupanda au kushuka Daraja na Kuongeza USIMAMIZI katika Michezo hiyo. TFF itakuwa na Vikao vya Kiutendaji na BODI ya Ligi,”.
    “TFF pia inavitaka Vilabu na Wadau wake wote halali wanaotaka kurekodi Michezo ya FDL na SDL (ambayo hakuna TV iliyo na HAKI za kuonesha kwa sasa) kuwasiliana na TFF na Kupata KIBALI kitakacholinda HAKI zao na za Mchezo (TFF) kabla ya kufanya hivyo. Ni Makosa kurekodi mchezo wowote kwenye Mashindano ya TFF bila IDHINI ya TFF,”.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YATAJA HATUA ILIZOCHUKUA JUU YA MECHI ZA DARAJA LA KWANZA ZILIZOLALAMIKIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top