• HABARI MPYA

    Thursday, January 04, 2018

    TANZIA: SURE BOY AFIWA NA MAMA YAKE MZAZI, MWANDISHI WA HABARI NAYE AFARIKI DUNIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIUNGO wa Azam FC, Salum Abubakar 'Sure Boy' (pichani kulia), amepata msiba mzito usiku wa kuamkia leo baada ya kufiwa na mama yake mzazi.
    Taarifa ya Azam FC leo imesema kwamba msiba upo Mtaa wa Lubusha, Magomeni jijini Dar es Salaam na mazishi yatafanyika leo saa 10 jioni.
    “Kwa niaba ya Uongozi, Bodi, wachezaji, mashabiki na wanafamilia wote wa Azam FC, tunapenda kutoa salamu zetu za rambirambi kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na marafiki,”.
    “Tunamuomba Mwenyezi Mungu amuepushe marehemu na adhabu ya kaburi, pia amfanyie wepesi Sure Boy katika kipindi hiki kigumu anachopitia.  Inna Lillahi Wa Inna Ilayhi Raji'un,”.
    Kwa msiba huu, mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Yanga SC, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ ameondoka kwenye kambi ya Azam FC kisiwani Zanzibar inaposhiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi kuja kushiriki mazishi ya mama yake mpendwa. 
    Naye mshambuliaji wa Reliants Lusajo amefiwa na baba yake mzazi usiku wa jana mjini Dar es Salaam. 
    Wakati huo huo: Mwandishi wa Habari za michezo wa muda mrefu, Athumani Hamisi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo mjini Dar es Salaam. 
    Athumani Hamisi alikuwa mwandishi mpiga picha wa magazeti ya The Guardian Limited kwanza, baadaye magazeti ya serikali, Daily News na Habari Leo.
    Lakini maisha yake ya kazi yalisitishwa na ajali aliyopata Agosti 12, mwaka 2008 Kibiti mkoani Pwani akiwa kwenye msafara wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete katika ziara yake mikoa ya kusini.
    Marehemu Hamisi alipooza mwili mzima kabla ya kupelekwa kwa Afrika Kusini kwa matibabu na tangu hapo amekuwa akitumia baiskeli ya kiti maalum cha umeme kwa kuzunguka. Mungu awapumzishe kwa amani wapendwa wetu. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TANZIA: SURE BOY AFIWA NA MAMA YAKE MZAZI, MWANDISHI WA HABARI NAYE AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top