• HABARI MPYA

    Monday, January 08, 2018

    TAMBWE AREJESHWA DAR KWA MATIBABU YA MALARIA

    Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
    MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe amepanda boti mchana huu visiwani Zanzibar kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
    Daktari wa Yanga SC, Edward Bavu ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Tambwe amelazimika kuondoka kambini mjini Zanzibar kurejea Dar es Salaam kwa  ajili ya matibabu zaidi ya Malaria.
    “Ana Malaria, kwa siku zaidi ya nne sasa amekuwa na wakati mgumu, tumelazimika kumrejesha Dar es Salaam ili apatiwe matibabu zaidi,” amesema Dk. Bavu
    Tambwe anaondoka wakati Yanga SC leo inateremka Uwanja wa Amaan, Zanzibar kumenyana na Singida United kuanzia Saa 2:15 usiku.
    Amissi Tambwe amerejea mjini Dar es Salaam leo kwa ajili ya matibabu ya Malaria

    Mrundi huyo amekuwa katika msimu mgumu, akianza kukaa nje tangu Agosti kutokana na maumivu ya goti kabla ya kurejea Desemba, lakini mapema Januari hii tena anaondolewa kambini kwa sababu ya Malaria.
    Na hii inazidi kuipunguzia nguvu safu ya ushambuliaji ya Yanga kipindi hiki ambacho inawakosa wakali wake wengine wazoefu, Mzimbabwe Donald Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa. 
    Yanga sasa itaendelea kumtegemea Ibrahim Ajib pekee katika washambuliaji wazoefu kwenye hatua iliyobaki ya Kombe la Mapinduzi – zaidi ya hapo ni chipukizi akina Yohanna Oscar Nkomola, Juma Mahadhi na Matheo Anthony.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAMBWE AREJESHWA DAR KWA MATIBABU YA MALARIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top