• HABARI MPYA

  Saturday, January 13, 2018

  SIMBA SC KAMILI WAINGIA KAMBINI MOROGORO KUIKUSANYIA NGUVU SINGIDA UNITED

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  TIMU ya Simba SC imewasili mjini Morogoro kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Singida United Januari 18, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Simba SC imeweka kambi katika Chuo cha Biblia, Bigwa mjini Morogoro na leo jioni inaanza mazoezi kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkali kutokana na timu zote kuwa kwenye mbio za ubingwa.
  Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao kwa sababu ya mapumziko maalum aliyopewa kupata ahueni ya maumivu yake amepona na amerejea – naye pia yuko kambini mjini Morogoro.
  Kipa namba moja, Aishi Salum Manula aliyepewa ruhusa ya kwenda kuoa, kipa namba mbili Said Mohammed Nduda aliyekuwa majeruhi wote wapo kambini Morogoro.
  Na baada ya timu kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, viongozi wanatarajiwa kukutana na wachezaji kuwarudishia morali iliyopotea kabla ya mchezo na Singida.
  Ndani ya Simba inaaminika hakuna tatizo isipokuwa tu morali iliyopotea kutokana na mambo ambayo yanasuluhika na kuelekea kwenye Ligi Kuu, matarajio bado ni ubingwa kwa Wekundu wa Msimbazi.
  Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26, sawa na Azam FC, wakiizidi kwa pointi tatu Singida United na tano mabingwa watetezi, Yanga SC.
  Ligi Kuu inarejea leo baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha michuano ya kombe la Mapinduzi, inayofikia tamati leo usiku visiwani Zanzibar kwa mchezo wa fainali kati ya Azam FC na URA ya Uganda.       
  Mechi za leo; Lipuli wanaikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Samora mjini Iringa, Stand United wanaikaribisha Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na Ndanda FC watakuwa wenyejin wa Mbao FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara. 
  Kesho ni mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Janauri 15, Njombe Mji wataikaribisha Kagera Sugar FC Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na Janauri Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mzunguko wa 13 utahitimishwa kwa michezo miwili Januri 18, Simba wakiikaribisha Singida United Uwanja wa Taifa na Maji Maji wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KAMILI WAINGIA KAMBINI MOROGORO KUIKUSANYIA NGUVU SINGIDA UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top