• HABARI MPYA

  Tuesday, January 02, 2018

  SERIKALI YAINGILIA KATI UONEVU DARAJA LA KWANZA…YAIAGIZA TFF KUTENDA HAKI HARAKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameshtushwa na kusikitishwa na malalamiko ya wadau wa soka nchini kuhusu vitendo vya uonevu na upendeleo vinavyodaiwa kujitokeza katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
  Taarifa ya Wizara ya Habari imesema kwamba Waziri Mwakyembe ameliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuyafanyia kazi malalamiko hayo ili kujenga afya njema katika mchezo huo nchini. 
  Katika salamu zake za mwaka mpya kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, Waziri Mwakyembe amewataka viongozi wa TFF kuchukua hatua haraka kuchunguza kilichojiri katika mechi baina ya Dodoma FC na Alliance ya Mwanza mjini Dodoma na kati ya Pamba Mwanza na Biashara mjini Mwanza.
  Nani Coastal, nani Biashara? Rais wa TFF, Wallace Karia (kushoto) na Makamu wake, Michael Wambura (kulia)

  Waziri Mwakyembe amewataka TFF kuchunguza kwa undani kilichotokea katika mechi hizo na kutoa maamuzi ya haki bila kuangalia sura ya mtu ndani ya wiki hii bila kukosa.
  “Watanzania wana haki ya kujua kwa uwazi na ukweli msingi wa kadi nne nyekundu kutolewa kwa wachezaji wa timu moja katika mchezo mmoja, wanataka kujua kama kweli waandishi wa habari za michezo walizuiwa kufanya kazi yao ya kikatiba ya kuwataarifu Watanzania wenzao kuhusu michezo hiyo miwili na kama ni kweli, nani aliwazuia,”.
  “Wanataka kujua (Watanzania) kama vitendea kazi vyao viliharibiwa na muhusika alikuwa nani, wanataka kujua kauli ya makamisaa wa mechi hizo mbili, wanataka kujua faida ya kuendelea kuwa na Kamati ya Saa 72 na wanataja kujua hisia za ujumla za watazamaji siku hiyo kuhusu usimamizi wa michezo hiyo miwili,”Dk. Mwakyembe amesistiza katika salamu zake za mwaka mpya.
  Waziri Mwakyembe amesema pamoja na kwamba dhamana ya kusimamia na kuendesha mpira wa miguu imekasimiwa kwa TFF, kama Wizara wa sekta hiyo hawezi kukaa kimya wakati tuhuma nzito za upendeleo na milungula zinapoibuliwa, wakati TFF haishituki mara moja na kuchukua hatua haraka.
  “Tukiwa na mfumo mbovu uliosheheni mizengwe katika kupata timu bora za kupanda daraja kuingia Ligi Kuu, tusahau kuwa na Ligi Kuu yenye msisimko na ushindani mkali,”amesema Waziri Mwakyembe.
  Amewakumbusha viongozi wa TFF kuwa Watanzania wameupokea uongozi wao kwa imani, shauku na matarajio makubwa, hivyo wasiwavunje moyo kwa kigugumizi cha kujitakia katika maamuzi. Mwakyembe amewataka viongozi wa TFF kuipatia maelezo ya kina na ya dhati kila tuhuma wakianza na tuhuma za maendeleo na uonevu katika mechi mbili alizozitaja. 
  “Viongozi hawa wasipuuze na kudhani Watanzania hawajui, la hasha, wanajua sana ila wanawasogezea kamba pole pole viongozi hao wajinyonge wenyewe,” ameongeza.
  Waziri Mwakyembe amesema mathalani katika malalamiko aliyofikishiwa tangu Jumamosi iliyopita kuhusu mechi hizo mbili wananchi wanadai uwepo wa kampeni ya makusudi upande wa viongozi wa TFF kuifanya timu ya Dodoma FC iingie Ligi Kuu kwa udi na uvumba.
  “Si dhambi kuiombea timu ya makao makuu ya nchi kuingia Ligi Kuu, lakini si sahihi hata kidogo kwa viongozi kuibeba timu hiyo kama madai hayo ni sahihi,”amesistiza.
  Aidha, taarifa ya Mwakyembe imesema kwamba tuhuma nyingine ambazo hazina uthibitisho zinauhusisha uongozi wa TFF kuibeba kuzibeba timu za Coastal Union na Biashara ya Musoma mkoani Mara. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERIKALI YAINGILIA KATI UONEVU DARAJA LA KWANZA…YAIAGIZA TFF KUTENDA HAKI HARAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top