• HABARI MPYA

    Thursday, January 04, 2018

    PRISONS YAPEWA USHINDI WA MEZANI ASFC, DROO YA 32 BORA KUPANGWA KESHO AZAM TV

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeipa ushindi Tanzania Prisons dhidi ya Abajalo FC wa mechi ya hatua ya 64 Bora michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) iliyoshindwa kufanyika Desemba 20, 2017  Uwanja wa Uhuru na Chamazi.
    Hiyo ni baada ya kikao chake cha Desemba 29, 2017 ukumbi wa makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume mjini Dar es Salaam kujadili mchezo namba 31 na 32 uliohusisha timu za Abajalo FC dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya na ule kati ya Mvuvumwa na JKT Ruvu katika Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iliyokuwa ifanyike Desemba 20, 2017 kwenye Uwanja wa Uhuru na Chamazi.
    Kamati ilikaa na kupitia taarifa mbalimbali za michezo hiyo na kupitia kanuni ya 24 kifungu cha (1) katika mchezo kati ya Abajalo FC na Tanzania Prisons imeipa ushindi timu ya Tanzania Prisons baada ya kubaini Abajalo kukiuka kanuni hiyo.
    Wachezaji wa Tanzania Prisons wamepta habari njema kwa kupewa ushindi wa mezani Azam Sports Federation Cup

    Kamati kupitia kanuni ya 24 kifungu cha (1) katika mchezo kati ya Abajalo FC na Tanzania Prisons imeipa ushindi timu ya Tanzania Prisons baada ya kubaini Abajalo kukiuka kanuni hiyo.
    Kwenye mchezo mwingine kati ya Mvuvumwa na JKT Ruvu Kamati baada ya kupitia na kujiridhisha imeipa ushindi timu ya JKT Ruvu baada ya Mvuvumwa pia kukiuka kanuni ya 24 kifungu (1).
    Kwa maamuzi hayo timu za Tanzania Prisons na JKT Ruvu zinafuzu kwenda kwenye hatua ya tatu(3) ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
    Wakati huo huo: Droo ya raundi ya tatu(3) ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) inachezeshwa kesho Januari 5, 2018 ikishirikisha timu 32.
    Raundi hiyo ya Tatu itahusisha timu nne(4) za mabingwa wa mikoa  timu tatu(3) za Ligi Daraja la Pili,timu Kumi na Mbili (12) za Ligi Daraja la Kwanza na timu 13 za Ligi Kuu.
    Hatua hiyo ya raundi ya tatu inabakiza timu Kumi na Sita(16) zitakazopambana kwenye hatua inayofuata.
    Timu zitakazochezeshwa kwenye Droo ya hapo kesho ambayo itarushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Azam ni pamoja na Buseresere ya Geita,Majimaji Rangers ya Lindi, Shupavu FC ya Morogoro na KariakooFC ya Lindi zote kutoka Ligi ya Mabingwa wa mikoa.
    Nyingine zinazotoka Ligi Daraja la Pili ni Green Warriors ya Dar es Salaam,Ihefu FC ya Mbeya na Burkina FC ya Morogoro.
    Zilizofanikiwa kuingia hatua hiyo kutoka Ligi Daraja la Kwanza ni Toto Africans ya Mwanza,KMC ya Dar es Salaam,Friends Rangers ya Dar es Salaam,Biashara ya Mara,Polisi Dar ya Dar es Salaam,Polisi Tanzania ya Kilimanjaro,,Rhino Rangers ya Tabora,JKT Oljoro ya Arusha,Pamba FC ya Mwanza na Dodoma FC ya Dodoma.
    Timu za Ligi Kuu zilioingia hatua hiyo ya raundi ya tatu ni Azam FC,Yanga(Dar es Salaam),Mtibwa Sugar ya Morogoro,Mbao FC ya Mwanza,Majimaji ya Songea,Kagera Sugar ya Kagera,Mwadui,Stand United (Shinyanga),Ruvu Shooting ya Pwani,Njombe Mji ya Njombe,Singida United ya Singida,Ndanda ya Mtwara na Tanzania Prisons ya Mbeya.
    Kamati ya nidhamu iliyokutana Januari 1, 2018 ilipitia ripoti mbalimbali za mchezo kati ya Kagera Sugar na Tanzania Prisons uliochezwa Uwanja wa Kaitaba Novemba 2, 2017 na ule kati ya Azam Fc na Mbeya City uliochezwa Uwanja wa Chamazi Oktoba 27, 2017.
    Kwenye mchezo kati ya Kagera Sugar na Tanzania Prisons,Meneja wa timu ya Tanzania Prisons Erasto Ntabahani alipelekwa kwenye kamati hiyo ya nidhamu kwa kosa la kumshambulia muamuzi wa akiba,kamati imejiridhisha kuwa Ntabahani alimshambulia kwa maneno muamuzi huyo wa akiba na hivyo imemfungia miezi miwili(2) na kulipa faini kwa mujibu wa kanuni ya 40(2) ya udhibiti wa viongozi.
    Kamati pia ilipitia suala la golikipa wa Mbeya City Owen Chaima kudaiwa kumpiga mshambuliaji wa Azam FC Yahya Mohamed.
    Chaima alikiri kumpiga Yahya na Kamati kupitia kanuni ya 35(7b) ya udhibiti wa wachezaji imemfungia kucheza mechi 4 na faini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PRISONS YAPEWA USHINDI WA MEZANI ASFC, DROO YA 32 BORA KUPANGWA KESHO AZAM TV Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top