• HABARI MPYA

  Monday, January 08, 2018

  NI YANGA NA URA, AZAM FC NA SINGIDA UNITED NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI JUMATANO ZANZIBAR

  Na Salum Vuai, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itakutana na URA ya Uganda katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Jumatano Uwanja wa Amaan, Zanzibar wakati Singida United itacheza na Azam FC.
  Hiyo ni baada ya Yanga kutoka sare ya 1-1 na Singida United katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi usiku huu Uwanja wa Amaan.
  Nusu Fainali ya kwanza itakuwa kati ya Yanga na URA Saa 10:30 jioni na saa 2:15 usiku Singida United na Azam zitachukua nafasi kwa mujibu wa ratiba kama hakutakuwa na mabadiliko.
  Upo uwezekano mkubwa, mchezo kati ya Azam FC na Singida ukatangulia jioni na Yanga na URA wakahamishiwa usiku.
  Katika mchezo usiku wa leo wa Kundi B, baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Singida United walitangulia kwa bao la mshambuliaji Daniel Lyanga dakika ya 72 aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu wa kiungo Kiggi Makassy kutoka nje kidogo ya boksi upande wa kushoto.
  Yanga wakasawazisha katika mazingira yale yale, mpira wa adhabu wa kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib kutoka upande wa kulia ulipounganishwa kwa kichwa na kiungo wa ulinzi, Said Juma ‘Makapu’ dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza kati ya tatu baada ya kutimia dakika 90 za kawaida za mchezo.
  Kwa ujumla ulikuwa mchezo mzuri ambao timu zote zilicheza kwa ustadi wa hali ya juu na kuwapa burudani watazamaji.
  Kocha Mholanzi Hans van der Plujim anafikisha mechi tatu bila kuifunga timu yake ya zamani, Yanga tangu ahame baada ya sare mbili za 1-1, ya mjini Singida mwaka jana na leo Zanzibar kufuatia kufungwa 3-2 Dar es Salaam kwenye mchezo wa kirafiki.
  Sifa ziwaendee makocha wasaidizi wa Yanga, Mzambia Noel Mwandila na mzalendo, Nsajigwa Shadrack Mwandemele kwa kuiongoza timu katika mechi nne bila kupoteza ikishinda nne na sare moja katika kipindi ambacho bosi wao, George Lwandamina yupo kwao, Zambia kwa matatizo ya kifamilia.     
  Mchezo wa kwanza wa kukamilisha mechi za Kundi A, Simba walichapwa 1-0 na URA hapa hapa Amaan na kesho watapanda boti kurejea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kikosi cha Singida United kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Michael Rusheshangoga, Shafiq Batambuze, Juma Kennedy, Malik Antiri, Yussuf Kagoma, Deus Kaseke, Mudathir Yahya/Kenny Ally dk75, Danny Lyanga, Kambale Salita Gentil/Lubinda Mundia dk75 na Kiggi Makassy. 
  Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Maka Edward/Said Juma ‘Makapu’ dk72, Pius Buswita/Matheo Anthony dk67, Raphael Daudi, Yohanna Nkomola/Juma Mahadhi dk67, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk76. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI YANGA NA URA, AZAM FC NA SINGIDA UNITED NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI JUMATANO ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top