• HABARI MPYA

  Saturday, January 13, 2018

  NI AZAM TENA, AU URA BINGWA MAPINDUZI LEO?

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  BINGWA wa Kombe la Mapinduzi 2018 anatarajiwa kupatikana leo baada ya mchezo wa fainali utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar baina ya Azam FC na URA ya Uganda.
  Azam FC ndiyo mabingwa watetezi wa Kombe hilo na watakutana na URA leo katika marudio ya mchezo wa Kundi A  Januari 5, 2018 ambao Watoza Kodi wa Uganda walishinda 1-0.
  Lakini siku hiyo, Azam FC ilipumzisha nyota wake wengi wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi na Simba ambayo ilichezwa siku iliyofuata tu, Janauri 6 na timu ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa ikashinda 1-0.
  Inatarajiwa kuwa fainali tamu kati ya fainali za Kombe la Mapinduzi zilizowahi kutokea, kwani URA na Azam FC zote zina vikosi na wachezaji bora kwa sasa.   
  Azam FC wataweza kubakiza Kombe la Mapinduzi nchini mbele ya URA ya Uganda leo? 

  URA iliongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya sare moja na kushinda mechi tatu, wakati Azam  FC ilifuatia kwa kushinda mechi tatu na kufungwa moja.
  Katika Nusu Fainali, URA iliing’oa Yanga kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90, wakati bao pekee la Shaaban Iddi Chilunda lilitosha kuipeleka Azam FC fainali kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United.  
  Hatimaye safari iliyoanza Desemba 29, mwaka jana inafikia tamati leo Uwanja wa Amaan kwa mchezo wa fainali, ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein.
  Jumla ya timu 11 zilishiriki michuano ya mwaka huu ambazo ni URA, Jamhuri, Mwenge, Azam na Simba zilizokuwa Kundi A na Zimamoto, Mlandege, Yanga, JKU, Taifa Jan’gombe na Singida United zilizokuwa Kundi B.
  Hizi ni fainali za 12 za Kombe la Mapinduzi na Azam FC watakuwa wanawania taji la nne la michuano hiyo baada ya awali kulitwaa katika miaka ya 2012, 2013 na 2017, wakati URA wao watakuwa wanawania taji la pili tu, baada ya awali kulitwaa mwaka 2016.
  Yanga SC ndiye bingwa wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2007 wakati watani wao wa jadi, Simba wamelitwaa mara tatu katika miaka ya 2008, 2011 na 2015. Timu nyingine zilizotwaa Kombe la Mapinduzi ni Miembeni 2009, Mtibwa Sugar 2010 na KCCA ya Uganda 2014.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI AZAM TENA, AU URA BINGWA MAPINDUZI LEO? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top