• HABARI MPYA

    Monday, January 08, 2018

    MWANASOKA BORA AFRIKA WA SAMATTA NI AUBAMEYANG

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba kura yake ya Mwanasoka Bora wa Afrika alimpigia Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon na klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online mwishoni mwa wiki, Samatta alisema anasikitika chaguo lake hilo halikushinda baada ya tuzo hiyo kuchukuliwa na nyota wa Misri na klabu ya Liverpool, Mohamed Salah.
    Salah, mwenye umri wa miaka 25, alipata pointi 625 katika jopo la wapiga kura linaloundwa na makocha wa timu za taifa na Manahodha pamoja na kikundi maalum cha Waandishi wa Habari na kuwashinda mchezaji mwenzake wa Liverpool, Msenegal Sadio Mane na Aubameyang kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Mbwana Samatta amesema kwamba Mwanasoka Bora wake wa Afrika na Pierre-Emerick Aubameyang

    “Chaguo langu lilikuwa Aubameyang, Salah nilimpa nafasi ya tatu baada ya Mane,”alisema Samatta ambaye kama Manahodha wengine wa timu za taifa barani, alipiga kura kwa njia ya email.
    Samatta na Aubameyang wanafahamiana vyema, baada ya wawili hao kukutana Januari mwaka juzi kwenye tuzo za Mwanasoka Bora Afrika mjini Lagos nchini Nigeria.
    Mwaka huo, Aubameyang alikuwa Mwanasoka Bora wa Afrika na Samatta akitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika baada ya mafanikio makubwa na TP Mazembe ya DRC akiipa taji la Ligi ya Mabingwa wa Afrika na kuwa mfungaji bora mwaka 2015.
    Mbwana Samatta (kushoto) akiwa na Pierre-Emerick Aubameyang Janauri 2016
    Na ni mwezi huo Januari 2016 Samatta alihamishia maisha yake ya kisoka Ulaya baada ya kununuliwa na KRC Genk y Ubelgiji anakoendelea na kazi hivi sasa akiwa tayari ni mchezaji muhimu.
    Lakini katika mastaajabu ya wengi, tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika ambayo Samatta alimuachia kipa Mganda wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Dennis Onyango aliyeshinda mwaka jana, haikuwepo mwaka huu.
    “Nastaajabu hata mimi, tuliletewa majina ya 10 Bora tu, baada ya hapo tukawa tunaletewa orodha nyingine nyngine tu, hiyo (Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika) majina yake hayakurudishwa,”alisema Samatta.
    Bado haijulikani sababu za CAF kutorejesha kipengele cha Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika, ambacho kilianzishwa baada ya kuona wachezaji wanaocheza barani wanafunikwa mno na wanaocheza Ulaya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWANASOKA BORA AFRIKA WA SAMATTA NI AUBAMEYANG Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top