• HABARI MPYA

  Thursday, January 11, 2018

  MAMA MKWASA AMTOLEA UVIVU CHIRWA, AMUAMBIA; ‘ALIIUA YANGA JANA ZENJI’

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MKE wa Charles Boniface Mkwasa, Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Beatrice Chalamila maarufu Betty Mkwasa amesema kwamba mchezaji Mzambia, Obrey Chirwa aliigharimu timu jana ikatolewa na URA kwenye Kombe la Mapinduzi.
  Yanga SC inarejea asubuhi ya leo mjini Dar es Salaam baada ya jana kutolewa kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapunduzi kwa penalti 5-4 na URA ya Uganda kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Chirwa alikosa penalti ya mwisho ya Yanga baada ya wenzake wote wanne, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi na wazalendo Hassan Ramadhani Kessy, Raphael Daudi Lothi na Gardiel Michael Mbaga kufunga.
  Obrey Chirwa (kulia) ameingia lawamani kwa kukosa penalti jana Zanzibar
  Tofauti na ilivyotarajiwa kwamba kuingia kwa Chirwa kwenda kuchukua nafasi ya Pius Buswita dakika ya 53 kungeiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya Yanga, lakini Mzambia huyo alishindwa kucheza vizuri kutokana na kile kilichoonekana wazi hakuwa fiti.
  Chirwa alikuwa kwao Zambia kwa zaidi ya wiki mbili kufuatia mgomo wake wa kushinikiza alipwe fedha za usajili na amerejea mapema wiki hii Dar es Salaam na moja kwa moja kusafirishwa kwenda Zanzibar kabla ya kuingizwa uwanjani kipindi cha pili jana.
  Na hata penalti aliyokwenda kupiga ilikuwa ya ovyo kabisa na kipa wa URA, Alionzi Nafian hakuhitaji kujisumbua kuiokoa, kwani mpira ulimkuta mikononi tena pale pale aliposimama. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Issa Hajji, aliyesaidiwa na Shehe Suleiman na Mwanahija Makame, penalti za URA zilifungwa na Patrick Mbowa, Enock Kigumba, Shafiq Kagimu, Jimmy Kulaba na Brian Majwega.
  URA sasa watakutana na Azam FC walioitoa Singida United jana kwa kuwachapa 1-0 katika Fainali Jumamosi Uwanja wa Amaan.
  “Leo ni kama Yanga walicheza pungufu uwanjani. (Chirwa) hakuwa na msaada wowote. Wakati fulani tuweke kando ushabiki tuzungumzie soka letu,” aliposti wenye ukurasa wake a Facebook Betty Mkwasa, Mkuu wa wilaya mbalimbali wa zamani nchini jana baada tu ya Yanga kutolewa na URA.
  Betty Mkwasa (kushoto) na Charles Boniface Mkwasa (kulia) 
  Betty ameshauri Yanga wajifunze kwa kosa la jana, kwani hakukuwa na haja ya kumchezesha Chirwa ambaye hakuwa na mazoezi na aliwasili jana hiyo hiyo Zanzibar.
  Betty amekerwa na kitendo cha wachezaji chipukizi waliofikisha timu hapo kutopewa nafasi jana. “Hata alipokosa penalti unaweza kuona kutoka kwenye sura yake, hakujali! Huu mtindo wa kuwathamini mapro (wachezaji wa kigeni) ambao wengi wao hujali zaidi maslahi kuliko kazi zao tuuache,”ameshauri. 
  “Angalia (Donald) Ngoma yuko wapi, angalia (Thabani) Kamusoko, ndio wale wale wenye migomo baridi. Tuache kusajili mapro kwa kushindana na Simba na Azam wenye fedha zao, tuwatumie yosso na wazalendo wetu ambao hadi sasa wameonyesha uwezo mkubwa,”alisema Betty jana.
  Charles Boniface Mkwasa (kushoto) wakati anamuona Betty Mkwasa (kulia) walipokuwa vijana wadogo miaka ya 1980 enzi hizo anachezea Yanga kabla ya kuwa kocha kocha na sasa kiongozi
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAMA MKWASA AMTOLEA UVIVU CHIRWA, AMUAMBIA; ‘ALIIUA YANGA JANA ZENJI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top