• HABARI MPYA

    Tuesday, January 02, 2018

    LIPULI WALALAMIKA WAAMUZI KUSABABISHA UGUMU USIOKUWEPO LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, IRINGA
    KOCHA wa Lipili FC ya Iringa, Amri Said amesema kwamba hakuna ushindani wowote katika timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zaidi ya changamoto za marefa kuhofia kazi kiasi cha kutofuata sheria 17 za soka ndio zinasababisha ugumu huo.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini hapa, Amri amesema kwamba imekuwa inaonekana kama Ligi Kuu ina ushindani mkubwa na ndiyo maana timu zote 16 haziachani sana kwenye msimamo wa Ligi Kuu, lakini ukweli ni kwamba marefa ndiyo wanaharibu mchezo.
    ‘’Ugumu wa ligi hii hauletwi na kupambana kwa timu, ila unnaletwa na waamuzi kuweka usawa katika mchezo, wanaona utakuwa mgumu kwa upande wao hivyo wanaamua kufanya kila mbinu kuhakikisha mchezo unamalizika kwa sare ili mashabiki wa soka wasilalamike kutokana uchezeshaji wao,”amesema.
    Akizungumzia timu yake kupata sare kwenye michezo miwili dhidi ya vigogo, Simba na Yanga Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Saalam, Amri amesema walicheza mpira kila mtu aliona na mwamuzi hakuweza kufanya hujuma kwa sababu yeye mwenyewe aliona timu yao inacheza soka la kuvutia na kuwapa shida wakongwe hapa nchini hadi kuambulia sare katika mechi hizo.
    ‘’Lipuli ni klabu ya tofauti sana kwa soka la Tanzania na ina malengo ya kutaka kuonyesha kuwa ina uwezo wa kubadilisha taswira ya ligi kuu Tanzania Bara ndiyo maana mimi na mwenzangu, Suleiman Matola tumejipanga kufanya hivo na naamini tutafanikiwa, kwani tuna wachezaji vijana wenye uwezo wa kucheza mpira kwa vipaji vya hali ya juu wakipewa nguvu na hawa kina Malimi Busungu, tutafanikiwa,”amesema.
    Lipuli FC inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 14 sawa na Mbao FC walio nafasi ya saba, baada ya kucheza mechi 12. Lipuli inazidiwa pointi 12 na vinara Simba na Azam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIPULI WALALAMIKA WAAMUZI KUSABABISHA UGUMU USIOKUWEPO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top