• HABARI MPYA

  Sunday, January 07, 2018

  KWA MADUDU HAYA, SOKA YA TANZANIA BADO INA SAFARI NDEFU

  SENEGAL watashiriki tena fainali za Kombe la Dunia mwaka huu nchini Urusi baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 2002 Korea Kusini na Japan.
  Majina kama Tony Sylva, Ferdinand Coly, Lamine Diatta, Papa Malick Diop, Omar Daf, Aliou Cisse aliyekuwa Nahodha, Moussa N'Diaye, Papa Bouba Diop, Salif Diao, Khalilou Fadiga na El Hadji Diouf chini ya kocha Mfaransa, Bruno Metsu yanakumbukwa mno kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 Senegal wakifika Robo Fainali.
  Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Afrika Kusini Uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane Novemba 14, mwaka jana ndiyo uliowarejesha Senegal Kombe la Dunia.
  Mabao ya Senegal yalifungwa na mshambuliaji wa West Ham, Diafra Sakho dakika ya 12 na Thamsanqa Mkhize aliyejifunga dakika ya 38.
  Ikumbukwe huo ulikuwa mchezo wa marudio, baada ya ushindi wa 2-1 wa Bafana Bafana Novemba 12 mwaka juzi kutenguliwa na kuamriwa mechi irudiwe, kufuatia refa Joseph Lamptey kufungiwa maisha na Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). 
  Ikumbukwe Septemba 7, mwaka huu, Idara ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 ya FIFA, iliagiza mchezo kati ya Afrika Kusini na Senegal uliofanyika Novemba 12, mwaka 2016 urudiwe baada ya kumkuta Lamptey na hatia ya kupanga matokeo ili kuibeba Afrika Kusini.
  Bafana Bafana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi y Simba wa Teranga Novemba mwaka juzi, lakini ikabainika walimtumia refa kupanga ushindi huo.
  Uamuzi huo unafuatia uthibitisho wa Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kuafiki kifungo cha maisha cha refa Joseph Lamptey wa Ghana kwa kuvurunda kimaamuzi katika mchezo huo, hivyo kuadhibiwa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA kabla ya kukata Rufaa iliyodunda Kamati ya Rufaa. 
  Na baada ya mchezo huo kurudiwa Novemba 14, mwaka jana, Senegal wanafuzu Kombe la Dunia, nafasi ambayo waliipata kuipigania haki yao nje ya Uwanja.
  Nchini Tanzania marefa wote wanne waliochezesha mechi namba 39 ya Kundi C Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kati ya Dodoma FC iliyoshinda 3-2 dhidi ya Alliance Schools wamefungiwa kwa kuchezesha chini ya kiwango.
  Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, maarufu Kamati ya Saa 72 kilichofanyika Januari 4, mwaka huu mjini Dar es Salaam kujadili mechi mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili.
  Waamuzi waliofungiwa ni Andrew Shamba, Abdallah Mkomwa, Athuman Athuman na Omari Juma ambao kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka mitatu kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
  Kamisaa wa mechi hiyo Mackshem T. Nzunda naye amefungiwa miaka mitatu kwa kushindwa kutoa taarifa ya mchezo kwa usahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 39(1) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Kamishna.
  Kamati imeomba suala la waamuzi hao ambao baadhi yao ni wa Ligi Kuu, kupitia TFF liwasilishwe kwenye chombo chenye dhamana ya kisheria ya rushwa kufanyiwa uchunguzi zaidi.
  Pamoja na hayo, Klabu ya Alliance Schools imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa timu yake kuonyeshwa kadi zaidi ya tano katika mechi hiyo iliyofanyika Desemba 30, 2017 mjini Dodoma. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42 (10) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti wa Klabu.
  Mchezaji Shaban William wa Alliance Schools amesimamishwa, hadi suala lake la kumpiga Mwamuzi litakaposikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF. Uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Usimamizi wa Ligi.
  Mapema kulikuwa kuna tuhuma za marefa hao kuwabeba Dodoma FC wakitoa kadi nyekundu tatu za uonevu kwa wageni na kuongeza muda kuwapa nafasi wenyeji kupata mabao na kutoka na nyuma kwa 2-1 hadi kushinda 3-2. 
  Kitendo cha Kamati kuwafungia marefa na Kamisaa kwa kipindi kirefu kinadhihirisha walivuruga mchezo na agizo la marefa hao kupelekwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) linaashiria mambo sawa na yaliyotokea kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia kati ta Senegal na Afrika Kusini.
  Lakini pamoja na mapungufu yote ya waamuzi yaliyovuruga mchezo huo, matokeo hayajatenguliwa na zaidi Alliance imeadhibiwa kwa kadi nyekundu tatu na njano mbili walizoonyeshwa na marefa ambao tayari imeonekana walivurunda na wametiliwa shaka ya rushwa.
  Kwa kesi hizi mbili unapata picha halisi ya soka ya Tanzania na kiini cha matatizo yake – unaona kabisa mpira wa miguu wa nchi hii una safari ndefu kufika kwenye mwanga wa mafanikio.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KWA MADUDU HAYA, SOKA YA TANZANIA BADO INA SAFARI NDEFU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top