• HABARI MPYA

    Monday, January 01, 2018

    KIYOMBO: WAKATI UKIFIKA NITAITWA TAIFA STARS, NDOTO ZANGU KUCHEZA ULAYA

    Na Abdallah Chaus, MWANZA
    MFUNGAJI wa mabao ya Mbao FC katika ushindi wa 2-0 dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC jana kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Habib Hajji Kiyombo (pichani kushoto) amesema kwamba anaamini wakati utafika ataitwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana kwa furaha ya kufunga mabao yote timu yake ikiwaadhiri vigogo hao, Kiyombo alisema kwamba muda wake wa kuitwa kwenye kikosi cha kocha Salum Mayanga wa Taifa Stars haujafika.
    “Muda bado ndio maana hadi leo mwalimu hajaniita, muda ukifika nitaitwa tu bila shida yoyote. Kila kitu kina muda wake, kwangu mimi suala la kuitwa timu ya taifa siwezi kuongea mengi, kwani naamini muda wangu haujafika na nina uhakika ukifika nitakwenda kulitumikia taifa langu bila wasiwasi na kuiletea heshima Tanzania katika eneo la ushambuliaji,”amesema.
    Kiyombo amesema msimu huu anataka apambane na washambuliaji wa kigeni ambao wamekuwa wakitamba kwa mabao katika Ligi Kuu na kwamba ndoto zake ni kucheza Ulaya ndiyo maana anajibidiisha kuhakikisha anakuwa mfungaji mzuri.
    “Mimi nina ndoto ya kucheza Ulaya ili badaye nije nililetee heshima taifa langu, kwani naamini uwezo huo ninao na kipaji ninacho na nina imani Mungu atanisaidia nitafanikiwa juu ya hilo,”amesema.
    Katika hatua nyingine, Kyombo amesema hana mawazo ya kuondoka Mbao FC kwa sasa kwa sababu anaipenda klabu yake na anawaheshimu viongozi na mashabiki wa timu hiyo iliyompatia umaarufu.
    “Bila Mbao watu wasingenifahamu, kama itatokea kuondoka Mbao FC sitojisikia furaha kucheza dhidi ya timu yangu, kikubwa ninawaomba mashabiki wa Mbao waendelee kunipa ushirikiano, kwani naamini nitafanya ninachokitaka,”amesema.
    Kiyombo aliyefunga mabao matano katika ushindi wa 5-1 wa Mbao FC kwenye hatua ya 64 Bora michuano ya Azam Sports Fedreration Cup (ASFC) dhidi ya Makanyagio huko Sumbawanga mkoani Katavi wiki mbili zilizopita, kwa sasa anashika nafasi ya pili kwa ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu kwa mabao yake saba, akizidiwa moja tu na mshambuliaji wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIYOMBO: WAKATI UKIFIKA NITAITWA TAIFA STARS, NDOTO ZANGU KUCHEZA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top