• HABARI MPYA

  Friday, January 12, 2018

  ALIYEIPELEKA AZAM FAINALI MAPINDUZI ASEMA KOMBE LINABAKI CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Shaaban Idd Chilunda anaamini ya kuwa watabeba kwa mara ya pili mfululizo uingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa URA ya Uganda kwenye mchezo wa fainali utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar kesho Saa 2.15 usiku.
  Idd aliiwezesha Azam FC kutinga hatua hiyo juzi baada ya kufunga bao pekee kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi Singida United ulioisha kwa matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex kushinda bao 1-0.
  Mwaka jana Azam FC yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Simba 1-0 kwenye fainali, bao pekee la Nahodha Himid Mao ‘Ninja’ kwa shuti kali la mbali lililomshinda kipa Mghana Daniel Agyei.
  Shaaban Idd anaamini Azam FC watabeba kwa mara ya pili mfululizo Kombe la Mapinduzi Jumamosi ya kesho

  Idd amesema kwamba mchezo huo wa fainali utakuwa mgumu, lakini anamuamini Mungu, wachezaji wenzake, makocha na timu hiyo watafanya vizuri na kuweza kutwaa tena taji hilo.
  “Mechi si rahisi kama inavyofikiriwa (vs URA), mechi ni ngumu kama uliona mechi ya kwanza tuliocheza nao kwenye hatua ya makundi waliweza kutufunga kwa hiyo mechi ya fainali nayo haitakuwa rahisi, lakini namwamini Mwenyezi Mungu, namuamini kocha wetu, nawaamini wachezaji wenzangu na timu yetu tutaweza kufanya vizuri na kuchukua tena ubingwa,” alisema.
  Katika hatua nyingine, Idd alimshukuru Mwenyezi kwa kuipeleka timu hiyo fainali na kuwaambia mashabiki wa Azam FC wamuombee na kuendelea kumpa sapoti baada ya kurejea tena dimbani akitokea kwenye majerahi.
  “Naishukuru sana timu yangu ya Azam FC kwa kuweza kunitibia vizuri mpaka hatimaye leo nimeweza kurudi, kama mnavyoona sichezi dakika nyingi kutokana na ripoti ya daktari inavyoeleza natumia dakika chache, lakini dakika hizo nimeweza kuzitumia kuisaidia timu yangu, afya yangu ikizidi kuwa vizuri nitafunga mabao mengi na kupata muda mwingi wa kucheza,” alisema.
  Mshambuliaji huyo alikuwa nje kwa takribani miezi mitano tokea msimu uliopita ulivyomalizika na kwa mara ya kwanza ameanza kuonekana dimbani tena kwenye michuano hii ya Mapinduzi wakati Azam FC ikiifunga Mwenge mabao 2-0 katika mchezo wa makundi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ALIYEIPELEKA AZAM FAINALI MAPINDUZI ASEMA KOMBE LINABAKI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top