• HABARI MPYA

  Saturday, December 09, 2017

  ZANZIBAR HEROES WATINGA NUSU FAINALI CHALLENGE BAADA YA SARE YA 0-0 NA WENYEJI, KENYA

  Na Mwandishi Wetu, MACHAKOS
  ZANZIBAR imekuwa timu ya kwanza kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Kenya katika mchezo wa Kundi A jioni ya leo Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos, Kenya.
  Matokeo hayo yanamaanisha, Zanzibar inafikisha pointi saba baada ya kucheza mechi tatu, ikishinda mbili 3-1 dhidi ya Rwanda na 2-1 dhidi ya Tanzania Bara kabla ya sare ya 0-0 leo na Kenya – na itaingia kwenye mchezo wa mwisho wa kundi lake dhidi ya Libya Desemba 11 kutafuta kulinda rekodi yake ya kutopoteza mechi.
  Timu hiyo ya kocha Hemed Morocco, kwa mara nyingine leo imeonyesha mchezo mzuri, lakini tu bahati haikuwa yao kupata goli.
  Kwa kiasi kikubwa kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa Zanzibar Heroes ambao walipambana kuhakikisha wanawadhibiti vema wapinzani wao.
  Kenya walilisakama zaidi lango la Heroes, lakini umakini wa kipa wa Zanzibar na safu yake ya Ulinzi waliweza kuondosha hatari kadhaa.
  Mapema katika mchezo mwingine wa Kundi A uliotangulia leo mchana, Tanzania Bara ilipoteza nafasi ya kwenda Nusu Fainali baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Rwanda Uwanja wa Kenyatta pia.
  Bara wanakamilisha mechi tatu bila ushindi, wakiwa wamepoteza mbili wakifungwa 2-1 zote dhidi ya Zanzibar na Rwanda baada ya kuanza kwa sare ya 0-0 na Libya na sasa watakamilisha mechi zao kwa kumenyana na Kenya Desemba 11 kabla ya kurejea nyumbani. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZANZIBAR HEROES WATINGA NUSU FAINALI CHALLENGE BAADA YA SARE YA 0-0 NA WENYEJI, KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top