• HABARI MPYA

    Saturday, December 09, 2017

    STARS YAGEUZWA ‘GUNIA LA MAZOEZI’ KENYA, YAPIGWA 2-1 NA RWANDA

    Na Mwandishi Wetu, MACHAKOS
    TANZANIA Bara imepoteza matumaini ya kwenda Nusu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Rwanda leo Uwanja wa Jomo Kenyatta mjini Machakos, Kenya.
    Kipigo hicho kinamaanisha Kilimanjaro Stars imekwishatolewa na sasa itaingia kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya wenyeji, Kenya Desemba 11 kukamilisha ratiba – na pia kujaribu kulinda heshima japo kwa kushinda mechi moja.
    Bara ilianza michuano kwa sare ya 0-0 na Libya kabla ya kufungwa 2-1 na Zanzibar na leo pia kuongezwa 2-1 nyingine na Rwanda.
    Nahodha wa Kilimanjaro Stars, Himid Mao Mkami ameshindwa kuisaidia timu yake Machakos


    Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Amavubi wakitangulia kwa bao la Innocent Nshuti dakika ya 17, kabla ya Danny Lyanga kuisawazishia Kili Stars dakika ya 37.

    Kipindi cha pili, Rwanda walirudi na maarifa mapya na nguvu zaidi hadi kufanikiwa kupata bao la ushindi lililofungwa na Abeid Biramahire dakika ya 65 akimalizia krosi ya Omborenga Fitina.
    Kilimanjaro Stars inayofundishwa na Ammy Ninje ilipambana mno kusaka bao la kusawazisha, lakini waliishia kupoteza nafasi chache walizotengenza.
    Mchezo wa pili wa Kundi A kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Zanzibar ndiyo unaoendelea sasa.  
    Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Aishi Manula, Himid Mao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Wilson, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Abdul Hilal/Shiza Kichuya dk72, Raphael Daudi, Danny Lyanga, Yahya Zayed/Yohanna Nkomola dk75 na Ibrahim Ajib.
    Rwanda; Marcel Nzarora, Thiery Manzi, Ali Mbogo, Soter Kayumba, Fitina Omborenga, Amran Nshiyimana, Djihad Biziman, Eric Rutanga, Muhadjiri Hakizimana, Justin Mico na Innoncent Nshuti. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YAGEUZWA ‘GUNIA LA MAZOEZI’ KENYA, YAPIGWA 2-1 NA RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top