• HABARI MPYA

    Friday, December 08, 2017

    STARS KUMKOSA YONDAN DHIDI YA RWANDA KESHO MACHAKOS, MBARAKA AREJEA

    Na Mwandishi Wetu, MACHAKOS
    BEKI wa kati wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Kelvin Yondani ataukosa mchezo wa Kundi A Kombe la CECAFA Challenge kesho dhidi ya Rwanda Uwanja wa Kenyatta, Machakos nchini Kenya.
    Yondani amepewa mapumziko ya siku tatu baada ya kuumia kifundo cha mguu kwenye mchezo wa jana dhidi ya Zanzibar, Bara ikichapwa 2-1.
    Hivyo atakosa mchezo huo wa kesho ukiwa ni miongoni mwa mechi mechi za michuano ya kuwania Kombe la Afrika Mashariki maarufu kama Cecafa Senior Challenge inayofanyika hapa Kenya.
    Jopo la Madaktari wa Kilimanjaro Stars linaloundwa na Dk. Richard Yomba na Dk Gilbert Kigadye limethibitisha kuwa majeraha aliyoyapata Yondani sio makubwa na yanahitaji apumzike kwa saa 72 ambazo ni sawa na siku tatu.
    Kelvin Yondani ataukosa mchezo dhidi ya Rwanda kesho Uwanja wa Kenyatta, Machakos nchini Kenya

    Vipimo vilivyochukuliwa vinaonesha kuwa hakuna mfupa wowote ulioathirika zaidi ya kupata mshtuko kiasi kwa hiyo wamempa siku tatu za mapumziko wakiendelea kumtazama maendeleo yake kwa ukaribu.
    Kwa upande wa Mbaraka Yusuph ambaye alipata majeraha ya misuli kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Libya, amepona na anatarajia kuingia kwenye program ya utimamu wa mwili.
    Hata hivyo Mbaraka hataweza kucheza kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Rwanda.
    Wakati huo huo, leo kikosi cha Kilimanjaro Stars kimefanya mazoezi kwenye Uwanja wa Machakos Academy licha ya mvua zinazoendelea kunyesha hapa County ya Machakos.
    Kilimanjaro inajiandaa na mchezo wa kesho dhidi ya Rwanda utakaochezwa saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos.
    Mchezo huo wa kundi A una umuhimu mkubwa kwa Kilimanjaro Stars katika harakati zake za  kuitafuta tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali.
    Kilimanjaro Stars ina pointi moja mpaka sasa baada ya kutoka sare na Libya kwenye mchezo wa kwanza kabla ya kufungwa na Zanzibar kwenye mchezo wake wa pili.
    Kundi A linaongozwa na  Zanzibar wenye pointi sita (6) wakifuatiwa na Uganda wenye pointi (4) wakati Libya yenyewe ina pointi (3) ikikamata nafasi ya tatu ikifuatiwa na Kilimanjaro Stars na Rwanda wenye pointi (1) kila mmoja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS KUMKOSA YONDAN DHIDI YA RWANDA KESHO MACHAKOS, MBARAKA AREJEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top