• HABARI MPYA

    Tuesday, December 05, 2017

    STARS KUMKOSA MBARAKA YUSUPH MECHI NA ZANZIBAR KESHOKUTWA

    Na Mwandishi Wetu, MACHAKOS
    MSHAMBULIAJI wa Tanzania Bara, Mbaraka Yusuph hataweza kucheza mechi ijayo ya Kundi A Kombe la Challenge dhidi ya Zanzibar Desemba 7, mwaka huu baada ya jana kushindwa kufanya mazoezi kutokana na maumivu ya misuli.
    Hayo yamethibitishwa na kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Ammy Conrad Ninje alipozungumza na Waandishi wa Habari nchini Kenya jana ambako michuano ya Challenge inafanyika mwaka huu.  
    Mbarak Yusuph ndiye mchezaji pekee ambaye hakufanya mazoezi jana baada ya kuumia misuli kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A juzi dhidi ya Libya timu zikitoka sare ya 0-0.
    Mbaraka Yusuph aliumia katika mchezo dhidi ya Libya juzi Uwanja wa Kenyatta mjini Machakos

    Baada ya sare ya 0-0 na Libya juzi, Kilimanjaro Stars itarudi uwanjani keshokutwa kumenyana na ndugu zake, Zanzibar kabla ya Desemba 9 kucheza na Rwanda na Desemba 11 kukamilisha mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya.
    Ninje amepanga kutumia mazoezi ya leo kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye mchezo dhidi ya Libya ili timu ipate matokeo mazuri kwenye mechi zijazo.
    Ninje amesema katika mchezo huo wa kwanza walicheza katika kiwango cha kuridhisha na kikubwa anataka kuangalia namna ya kufanyia kazi upungufu ikiwa ni pamoja na pale timu inapopoteza mpira.
    Anasema kwenye mchezo dhidi ya Libya timu ilicheza kuanzia nyuma kupitia sehemu ya kiungo na kuunganisha sehemu ya ushambuliaji – jambo ambalo limemfurahisha kwa namna timu ilivyotengeneza nafasi.
    Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Zanzibar Heroes, Ninje amesema ni mchezo mgumu kama ambavyo historia inaonesha wakati timu hizo mbili zinapokutana.
    “Lakini kuanzia mazoezi ya kesho nitaiandaa timu kupata ushindi na nimepanga kwenda kuitazama Zanzibar itakapocheza mchezo wake wa kesho dhidi ya Rwanda,” amesema.
    Amesema ataiangalia Zanzibar Heroes kiufundi ili kubaini upungufu wao ili naye ajue namna atakavyoweza kutumia nafasi hizo kwenye mchezo unaofuata.
    “Ni fahari kwa timu zetu hizi mbili kila mmoja kupambana kupata pointi bahati nzuri wao wanacheza kesho kwa hiyo mchezo wao nitautumia kutazama mapungufu (upungufu wao) yao yatakayoweza kutusaidia,’’ alisema Ninje.
    Kilimanjaro Stars ipo kundi A pamoja na timu za Zanzibar, Libya, Rwanda na wenyeji Kenya.
    Kenya wana pointi tatu baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 wakati Kilimanjaro Stars na Libya wana pointi 1 kila mmoja baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwenye mchezo wao wa kwanza wakati Zanzibar na Rwanda wenyewe hawana pointi huku Zanzibar ikiwa haijashuka dimbani katika kundi hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS KUMKOSA MBARAKA YUSUPH MECHI NA ZANZIBAR KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top