• HABARI MPYA

    Thursday, December 14, 2017

    SAMATTA: NINAENDELEA VIZURI NAMSHUKURU MUNGU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba anafurahi hali yake inaendelea kuimarika vizuri na ni matarajio yake kurejea uwanjani mapema kabisa Januari. 
    Mchezaji huyo wa KRC Genk ya Ubelgiji kwa sasa anaendelea na mazoezi ya gym kwa bidii katika kupambana na maumivu yake ya goti.
    Akizunguma na Bin Zubeiry Sports – Online leo kutoka Genk, Samatta amesema kwamba anaendelea vizuri na goti lake kiasi kwamba anaamini atarejea uwanjani akiwa imara zaidi.
    “Poa, ninaendelea vizuri kabisa namshukuru Mungu, bado nipo kwenye mazoezi ya gym”amesema Samatta aliyefanyiwa upasuaji wa goti hilo Novemba 10 mjini Genk, Ubelgiji.
    Mbwana Samatta anafurahi hali yake inaendelea kuimarika vizuri na anatarajia kurejea uwanjani mapema Januari 

    Samatta amekamilisha wiki nne kati ya sita za mapumziko kufuatia kuumia Novemba 4, mwaka huu akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Na baada ya kufanyiwa vipimo iligundulika Samatta aliumia kwenye mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia ambayo ilichanika, hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji mdogo ili apone sawia.
    Samatta aliumia akiichezea mechi ya 70 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Na katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: NINAENDELEA VIZURI NAMSHUKURU MUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top