• HABARI MPYA

  Saturday, December 09, 2017

  RAIS MAGUFULI AWASAMEHE BABU SEYA NA PAPII KOCHA

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Joh Pombe Joseph Magufuli ametangaza kuwasamehe mwanamuziki Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanawe, Papi Kocha, waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha gerezani.
  Akihutubia taifa katika sherehe za Uhuru mjini Dodoma leo, Rais Magufuli pia ametangaza kuwasamehe wafungwa wengine 8,157, na kuagiza wafungwa 1,828 kati yao watolewe magerezani mara moja na waliobaki wapunguziwe muda wa kukaa gerezani ili waje kutolewa kwa mujibu wa vifungo vyao.
  Pia ametangaza kuwasamehe wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa, na kuagiza watolewe gerezani leo au kesho.

  Babu Seya (kulia) na mwanawe, Papii Kocha (kushoto) wakiwapungia mikono mashabiki wao waliojitokeza kuwalaki wakati wanaachiwa kwa msamaha wa Rais

  Kuhusu waliohukumiwa kunyongwa, Rais Magufuli ametoa mifano kwa kusema; “Yuko mtu aliyefungwa akiwa na miaka 18, na sasa hivi ana miaka sitini na kitu. Yumo mtu anaitwa Mganga Matonya, ana miaka 85 na ameishakaa gerezani miaka 44,”.
  Nguza na wanawe watatu, akiwemo Nguza Mbangu na Francis ‘Chichi’ Nguza walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa Kituo cha Polisi Magomeni, Dar es Salaam kwa tuhuma za kuwanajisi watoto 10 eneo la Sinza Mapambano.
  Walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Oktoba 16, mwaka 2003 wakituhumiwa kubaka na kunajisi watoto 10 waliokuwa wanafunzi na jirani zao.
  Baada ya kusikilizwa kesi hiyo Juni 25, 2004, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya aliwatia hatiani Babu Seya na wanawe kwenda jela maisha kwenye Gereza la Ukonga, Dar es Salaam.
  Januari 27, mwaka, 2005, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu.
  Awali mwaka 2004, baada ya kukutwa na hatia katika kesi hiyo, Babu Seya, Papii Kocha na wakili wao, Mabere Nyaucho Marando walikata rufaa ya pili ambayo ilitupiliwa mbali.
  Mwaka 2010 waliomba tena rufaa ambayo marejeo yake yalisikilizwa na kutolewa hukumu Februari, 2010. Mahakama iliridhia hukumu ya kifungo cha maisha kwa Babu Seya na Papii Kocha, ikawaachia huru watoto wake, Mbangu na Francis Nguza.
  Na msamaha wao unakuja wakati tayari wamekata Rufaa Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCPHR) yenye makazi yake jijini Arusha ambayo, tayari ilikwishakutana  mara tatu na kubaini kuwa, hukumu ya Babu Seya na Papii ilikuwa na kasoro.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AWASAMEHE BABU SEYA NA PAPII KOCHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top