• HABARI MPYA

    Tuesday, December 05, 2017

    PLUIJM ANATAKA WASHAMBULIAJI WAWILI WAPYA SINGIDA UNITED IWE BALAA KABISA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Singida United, Mholanzi Hans van der Pluijm anataka kuongeza washambuliaji wawili kikosini, lakini kutoka hapa hapa nyumbani. 
    Pluijm, kocha wa zamani wa Yanga anaamini ana safu nzuri ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao matano tu katika mechi 11 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Lakini pia Pluijm anaamini mabao tisa ya kufunga katika mechi 11 si wastani mzuri, hivyo anahitaji kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji hivyo amependekeza wasajiliwe washambuliaji wapya wawili.
    Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba wakati kocha Pluijm anawapa muda zaidi washambuliaji wake wa kigeni, Mnyarwanda Danny Usengimana na Mzimbabwe Michelle Katsavairo anataka kusajili wazawa wawili.
    Hans van der Pluijm anataka kuongeza washambuliaji wawili Singida United

    “Wachezaji wengi wa kigeni wanapokwenda katika ligi mpya za nchi nyingine ni nadra kuanza na moto, mara nyingi huanza kufanya vizuri katika msimu wa pili, hivyo hata Pluijm bado ana imani sana na Usengimana na Katsavairo,”amesema Festo.
    Mkurugenzi huyo wa Singida amesema hata Mzambia Obrey Chirwa hakufanya vizuri msimu uliopita, lakini msimu huu umuhimu wake umeanza kuonekana Yanga SC. 
    Ikumbukwe Singida United jana imeachana na washambuliaji wazawa, Atupele Green na Pastory Athanas huku pia ikiwatoa kwa mkopo wachezaji wake wengine wawili, Mohamed Titi na Frank Zakaria kwenda Singida United wakiwa wamebakiza mwaka mmoja na nusu katika mikataba yao.  
    Singida United inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 20 ilizokusanya kwenye mechi 11, ikiziwa pointi tatu na vinara, Simba SC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PLUIJM ANATAKA WASHAMBULIAJI WAWILI WAPYA SINGIDA UNITED IWE BALAA KABISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top