• HABARI MPYA

  Thursday, December 07, 2017

  NGOMA APELEKWA KAMATI YA NIDHAMU, MKWASA ASEMA; ‘ANA KESI YA KUJIBU’

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  HATIMA ya mshambuliaji Mzimbabwe wa Yanga, Donald Dombo Ngoma inatarajiwa kujulikana mara baada ya kikao cha Kamati ya Nidhamu mapema wiki ijayo kitakachofanyika mjini Dar es Salaam.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Ngoma amewasilisha taarifa na vielelezo mbalimbali juu ya kuchelewa kwake baada ya kuruhusiwa kwenda kwao Zimbabwe mara moja.
  Hata hivyo, Mkwasa amesema kwamba suala la mchezaji huyo litajadiliwa na Kamati ya Nidhamu ya klabu kwa kuwa bado Ngoma alifanya makosa kuzidisha siku za ruhusa yake bila ya kuwasiliana na klabu.
  Donald Ngoma atafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu mapema wiki ijayo 

  “Pamoja na yote ataitwa kwenye kikao cha Kamati ya Nidhamu mapema wiki ijayo, suala lake litajadiliwa na baada ya hapo tutafikia suluhisho,”amesema.
  Aidha, Mkwasa amesema kwamba Kamati ya Usajili inatarajiwa kukutana pia mwishoni mwa wiki hii kupitia taarifa ya benchi la Ufundi chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina kuhusu wachezaji wa kuondolewa moja kwa moja, kutolewa kwa mkopo na wa kusajiliwa pia.
  Lakini Mkwasa alikataa kuthibitisha wala kukanusha kwamba kocha Lwandamina amependekeza viungo Said Juma ‘Makapu’, Yussuf Mhilu, Baruan Akilimali, Juma Mahadhi, Maka Edward na mshambuliaji Matheo Anthony waondoke wakacheze kwa mkopo klabu nyingine ili kukuza uwezo wao.
  “Ni kweli tuna taarifa imeletwa na kocha, lakini siwezi kuizungumzia kwa sasa hadi hapo Kamati ya Usajili itakapokutana mwishoni mwa wiki na kuifanyia kazi,”amesema Mkwasa. 
  Kuhusu Mzimbabwe mwingine, kiungo Thabani Kamusoko, Mkwasa amesema anaendelea na matibabu mjini Dar es Salaam, wakati mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe alikwenda kwao, Burundi kwa ruhusa maalum na anatarajiwa kurejea kuanzia leo.   
  Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam wakati huu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara imesimama kupisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inayoendelea nchini Kenya.
  Na Ligi Kuu ilisimama Yanga ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi zake 21 baada ya mechi 11, ikizidiwa pointi mbili na zote, Simba SC na Azam FC za Dar es Salaam pia.   
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGOMA APELEKWA KAMATI YA NIDHAMU, MKWASA ASEMA; ‘ANA KESI YA KUJIBU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top