• HABARI MPYA

    Thursday, December 07, 2017

    MWILI WA KOCHA BENDERA KUPUMZISHWA MILELE JUMAPILI KOROGWE

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    MWILI wa kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Dk. Joel Nkaya Bendera unatarajiwa kusafirishwa Jumamosi asubuhi kupelekwa nyumbani kwao, Korogwe mkoani Tanga kwa mazishi.
    Bendera aliyeiwezesha Tanzania kufuzu fainali pekee za Kombe la soka la Mataifa ya Afrika (AFCON), Joel Nkaya Bendera mwaka 1980 nchini Nigeria, alifariki dunia jana jioni katika hospitali ya taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
    Ratiba ya msiba wa Naibu huyo Waziri wa Michezo wa zamani inasema kwa sasa ndugu na jamaa wanaendelea kukutana nyumbani kwa marehemu, Sinza Dar es Salaam kwa maombolezo ambayo yataendelea hadi Jumamosi Saa 5.00 asubuhi mwili wake utakaposafirishwa kwenda Korogwe.
    Mwili wa Dk. Joel Bendera utasafirishwa Jumamosi asubuhi kupelekwa Korogwe mkoani Tanga kwa mazishi

    Mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumapili Saa 10.00 jioni baada ya ibada ya kuuombea mwili wa marehemu katika Kanisa la Mtakatifu Michael.
    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana alitoa salamu za rambirambi kufuatia msiba huo wa Bendera, kocha na Katibu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) enzi hizo likijulikana kama  FAT (Chama cha Soka Tanzania).   
    Bendera ambaye Mei 30, mwaka huu alifikisha umri wa miaka 67, umaarufu wake ulianzia kama kocha wa mpira wa miguu na alikuwa kocha wa timu ya taifa iliyofanikiwa kuitoa Zambia mwaka 1979 na kukata ya Fainali za AFCON mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Bendera akaendelea kuwa kocha miaka ya 1980 kabla ya kustaafu na kuhamia kwenye siasa ambako alianzia kwa kugombea ubunge wa jimbo la Korogwe mkoani Tanga mwaka 1995 na akafanikiwa kushinda.
    Bendera alilishikilia jimbo hilo hadi mwaka 2010 alipoangushwa kwenye kura za maoni za CCM na Abdallah Nassir Yussuf kwa tofauti ya kura 255 tu.  
    Akiwa Mbunge wa Korogwe, Bendera pia alikuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo tangu mwaka 2006 hadi 2010. Na ni kipindi hicho ambacho Tanzania ilipata tiketi ya kucheza Fainali za michuano mingine mikubwa Afrika, CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast, michuano inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
    Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Manyara, ambao umekuwa kituo chake cha mwisho cha utumishi wa umma kabla ya kukutwa na umauti. 
    Mungu ampumzishe kwa amani Mwalimu Joel Nkaya Bendera. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWILI WA KOCHA BENDERA KUPUMZISHWA MILELE JUMAPILI KOROGWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top