• HABARI MPYA

  Friday, December 15, 2017

  MSUVA ASIKITISHWA NA MATOKEO YA STARS KOMBE LA CHALLENGE, ASEMA; “TUTAJIPANGA UPYA”

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva anayechezea klabu ya Difaa Hassan El- Jadida ya Morocco, amesikitishwa na matokeo mabaya ya timu ya Bara katika michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya, lakini amesema watajipanga upya.
  Tanzania Bara ilipata sare moja tu, 0-0 na Libya na kufungwa mechi nyingine zote tatu za Kundi A Kombe la Challenge hivyo kutolewa mapema kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.
  Ilifungwa 2-1 mara mbili dhidi ya Zanzibar na Rwanda na 1-0 dhidi ya wenyei, Kenya na wakati michuano ipo kwenye hatua ya Nusu Fainali, tayari Kilimanjaro Stars ipo Dar es Salaam.
  Simon Msuva (kulia) akiwa na mchezaji mwenzake wa Difaa Hassan El- Jadida nchini Morocco, beki wa kati Bakary N'Diaye kutoka Mauritania 

  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu jana usiku kutoka Morocco, Msuva alisema kwamba amesikitishwa sana na matokeo hayo, kwani kwa kiasi kikubwa wachezaji wanaokuwa kwenye kikosi cha Bara ndiyo huunda Taifa Stars.
  “Ukitazama kikosi cha Challenge sana sana tumekosekana mimi, Banda (Abdi) na Kapteni wetu (Mbwana Samatta) ili kuwa Taifa Stars, maana yake hiyo ndiyo timu inayotegemewa kwa kampeni za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika. Kwa kweli ni mbaya sana,”amesema Msuva.
  Hata hivyo, mchezaji huyo wa zamani wa Yanga, amesema kwamba watajipanga upya baada ya matokeo hayo ya kusikitisha ili warejeshe heshima.
  “Haya mambo yanatokea katika soka wakati mwingine hata timu kubwa sana kama Brazil na Hispania zinapata matokeo ya kustaajabisha kabisa katika michuano, jambo la maana ni kujipanga upya,”amesema.    
  Msuva amewataka Watanzania kutokata tamaa na timu yao, bali kuendelea kuiunga mkono, kwani iko siku mambo yatakuwa mazuri. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MSUVA ASIKITISHWA NA MATOKEO YA STARS KOMBE LA CHALLENGE, ASEMA; “TUTAJIPANGA UPYA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top