• HABARI MPYA

  Wednesday, December 13, 2017

  LIPULI ‘WAIFUNGULIA MASHITAKA’ SIMBA KUMRUBUNI ASANTE KWASI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Lipuli ya Iringa imewasilisha barua ya malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya mchezaji wake, Mghana beki Asante Kwasi kufanya mazungumzo na klabu nyingine kinyume cha sheria.
  Barua hiyo iliyoelekezwa kwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao imedai kwamba Kwasi ameingia kwenye mazungumzo na klabu nyingine akiwa ndani ya mkataba na Lipuli, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
  “Wachezaji wengi wa Lipuli wamesajiliwa mwezi wa saba, nane, hivyo wana kipindi cha miezi mine ndani ya klabu. Hivyo kuanza, au kuongea nao juu ya usajili ni kinyume cha kanuni za usajili,”imesema barua ya Lipuli. 
  Asante Kwasi akiwa na jezi ya Simba kwenye mazoezini ya gym mapema wiki hii

  Katika barua yao kwenda TFF, Lipuli hawajaitaja klabu yoyote – lakini mapema wiki hii walikanusha kufanya mazungumzo ya aina yoyote na uongozi wa Simba SC ya Dar es Salaam kuhusu Mghana huyo aliyesajiliwa Julai mwaka huu kutoka Mbao FC ya Mwanza.
  Na hiyo ilifuatia kuvuja kwa picha ya Kwasi akifanya mazoezi gym akiwa amevalia jezi ya Simba katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajii.
  Afisa Habari wa Lipuli FC, Clement Sanga alisema kwamba hawajafanya mazungumzo yoyote na timu yoyote kuhusu mchezaji Asante Kwasi.
  “Ikumbukwe mchezaji Asante Kwasi licha ya uwepo wa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii bado ni mchezaji halali wa Lipuli FC. Kwasi bado ana si chini ya miezi saba kwenye mkataba wake wa sasa na Lipuli FC na kwa muktadha huo, bado ni mchezaji halali wa Lipuli FC,”amesema Sanga.
  Kwa sasa uongozi hauna mpango wowote wa kumuuza mchezaji huyo, si kwa Simba SC tu, bali pia kwa klabu nyingine yoyote na kama hapo baadaye kutatokea ulazima wa kufanya hivyo, uongozi utatoa taarifa.
  “Tunapenda kutoa ushauri wa bure kwa timu yoyote itakayoonyesha matamanio ya kumtaka mchezaji huyo kuwasiliana na uongozi wa Lipuli FC moja kwa moja ili kuepusha misuguano isiyokuwa na ulazima kwa afya ya familia ya mchezo wa soka nchini,”amesema Sanga.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LIPULI ‘WAIFUNGULIA MASHITAKA’ SIMBA KUMRUBUNI ASANTE KWASI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top