• HABARI MPYA

  Tuesday, December 12, 2017

  KANKU, NKOMOLA KUANZA KUICHEZEA YANGA DHIDI YA POLISI TZ JUMAMOSI UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI mpya wa Yanga, Mkongo Fiston 'Festo' Kayembe Kanku anatarajiwa kuichezea klabu hiyo kwa mara ya kwanza Jumamosi wiki hii itakapomenyana na Polisi Tanzania katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Pamoja na beki huyo kutoka Balende FC ya kwao, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo (DRC), siku hiyo Yanga pia inatarajiwa kumtumia kwa mara ya kwanza mshambuliaji wake mpya kinda wa miaka 17, Yohanna Oscar Nkomola ambao imewasijili mwezi uliopita kwa mikataba ya miaka miwili kila mmoja.
  Katika mchezo huo, kiingilio kinatarajiwa kuwa Sh. 10,000 kwa VIP A, 5,000 VIP B na 3,000 kwa majukwaa ya mzunguko.
  Fiston 'Festo' Kayembe Kanku anatarajiwa kuichezea Yanga kwa mara ya kwanza Jumamosi dhidi ya Polisi Tanzania  

  Baada ya mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa wiki mbili kupisha michuano ya CECAFA Challenge inayoendelea nchini Kenya, Yanga itacheza dhidi ya Polisi Tanzania Jumamosi.
  Kocha Mzambia, George Lwandamina anataka kutumia mchezo huo kukiseti kikosi chake kabla ya kurejea kwa mechi za Ligi Kuu.
  Yanga inakabiliwa na jukumu la kuzikimbiza Simba na Azam kileleni mwa Ligi Kuu, kwani baada ya mechi 11 mabingwa hao watetezi wamekusanya pointi 21, hivyo wanazidiwa pointi mbili na wapinzani wao hao.
  Yanga pia inatarajiwa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi mapema mwakani visiwani Zanzibar na imepangwa Kundi B pamoja na JKU, Mlandege, Zimamoto na Shaba, wakati Kundi A lina timu za Simba, Azam FC, Jamhuri, Taifa ya Jang’ombe na URA ya Uganda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KANKU, NKOMOLA KUANZA KUICHEZEA YANGA DHIDI YA POLISI TZ JUMAMOSI UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top