• HABARI MPYA

    Sunday, December 10, 2017

    KAMA NCHI HAINA WACHEZAJI BORA, TIMU BORA YA TAIFA ITATOKA WAPI?

    WIKI hii kiungo wa Singida United ya Singida, Mudathir Yahaya amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Novemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
    Mudathir ameshinda tuzo hiyo baada ya kuwazidi wenzake wawili, beki Asante Kwasi wa Lipuli ya Iringa na mshambuliaji Danny Usengimana wa Singida United pia, alioingia nao fainali ya kuwania nafasi hiyo.
    Katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii kwenye kikao cha Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
    Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United mwezi huo ikipata pointi saba katika michezo mitatu iliyocheza na kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita iliyokuwepo mwezi Oktoba hadi ya nne.
    Singida United ilitoka 0-0 na Yanga, iliifunga Mbeya City mabao 2-1 na pia iliifunga Lipuli bao 1-0, ambapo Mudathir anayecheza nafasi ya kiungo alicheza dakika zote 270 sawa na michezo mitatu na hakuwa na kadi yoyote.
    Alitajwa mchezaji bora wa mchezo wa Singida United na Yanga uliofanyika Uwanja wa Namfua, Singida, alicheza kwa kiwango cha juu wakati Singida United ilipochuana na Lipuli, pia alisaidia kutengeneza nafasi ambazo zilitumiwa vyema na wenzake katika kupata ushindi dhidi ya Mbeya City, huku yeye akihusika kwa kwa kiasi kikubwa kupambania ushindi huo.
    Mafanikio yake kwa mwezi huo yalisaidia kumrudisha katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na kile cha Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, ambacho kinashiriki michuano ya CECAFA Challenge inayoendelea nchini Kenya.
    Mudathir anakuwa mchezaji bora wa nne wa mwezi wa Ligi Kuu baada ya Waganda Emmanuel Okwi wa Simba mwezi Agosti na Shafiq Batambuze wa Singida United mwezi Septemba na Mzambia Obrey Chirwa wa Yanga mwezi Oktoba.
    Mudathir anakuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Ligi Kuu, baada ya wageni watatu mfululizo. Na ikumbukwe, mchezaji huyo anatokea visiwani Zanzibar ambako kwa miaka wapo kwenye harakati za kuomba uanachama wa FIFA.  
    Katika miezi yote minne ya awali, Ligi Kuu haijatoa mchezaji Bora wa mwezi mzawa wa Tanzania Bara na Mudathir anatangazwa mchezaji bora wa Novemba Ligi Kuu akiwa kwenye michuano ya CECAFA Challenge ambako tayari ameiwezesha Zanzibar Heroes kufika Nusu Fainali ikiwa timu ya kwanza kufanya hivyo.
    Zanzibar Heroes imekamatia pointi saba baada ya mechi mbili kutokana na kuzifunga Rwanda 3-1, Tanzania Bara 2-1 na sare ya 0-0 na wenyeji, Kenya jana hivyo kwenda Nusu Fainali mapema.
    Tanzania Bara haina nafasi ya kwenda Nusu Fainali baada ya kuambulia pointi moja katika mechi tatu, ikifungwa 2-1 zote na Zanzibar Heroes na Rwanda baada ya sare ya 0-0 na Libya.
    Tumeishuhudia Kilimanjaro Stars mbovu zaidi kwa muongo huu kwenye michuano ya Challenge chini ya kocha Ammy Conrad Ninje.
    Na baada ya matokeo hayo, wapenzi wa soka nchini wanaelekeza lawama zao kwa kocha Ninje kwamba ndiye chanzo cha timu kufanya vibaya wakihoji ujuzi, taaluma na uzoefu wake.
    Wengine wanakumbuka namna alivyoingia kwenye timu ya taifa kisanii mwaka 2003 chini ya kocha Profesa (wakati huo Dokta) Mshindo Msolla kama mchezaji akisema anatokea Reading ya England, ambako watu walipojaribu ‘kutafuta’ rekodi zake kama kweli ni mchezaji wa timu hiyo ‘hawakuona kitu’.
    Msolla hakushawishiwa na uwezo wa Ninje mazoezini, lakini mwenyewe mchezaji huyo akajigharamia usafiri kwenda na Taifa Stars nchini Malawi kwenye mechi ambako hakupata nafasi hata ya kuwekwa benchi.
    Na sasa Ninje amerudi Taifa Stars kwanza kama Kocha Msaidizi chini ya Salum Shaaban Mayanga kabla ya kufanikiwa kuwashawishi TFF wampe kikosi cha Kilimanjao Stars kama Kocha Mkuu.
    Inawezekana Ninje akawa tatizo, lakini anguko la Tanzania Bara kisoka linaanzia kwenye Ligi Kuu yake yenyewe ambako huko wachezaji wake hawafanyi vizuri.
    Kila klabu ya Ligi Kuu sasa inaruhusiwa kuwa na wachezaji saba wa kigeni kikosini na bado zina kiu ya kuongezewa wageni zaidi – kwa sababu haziridhishwi na wachezaji wa nyumbani.
    Inawezekana kufanya vibaya kwa Bara Challenge ni kutokana na kocha tunayeamini ‘bomu’ Ninje, lakini kabla ya kufika huko tuwatafakari na wachezaji wetu kwa sababu kama hauna wachezaji bora katika nchi huwezi kuwa na timu bora ya taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA NCHI HAINA WACHEZAJI BORA, TIMU BORA YA TAIFA ITATOKA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top