• HABARI MPYA

  Wednesday, December 06, 2017

  JOEL BENDERA AFARIKI DUNIA LEO MUHIMBILI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA aliyeiwezesha Tanzania kufuzu fainali pekee za Kombe la soka la Mataifa ya Afrika (AFCON), Joel Nkaya Bendera amefariki dunia jioni ya leo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.
  Msemaji wa hospital ya Muhimbili, Aminieli Eligaisha ameithibitishia Bin Zubeiry Sports – Online kufariki kwa Bendera aliyewahi pia kuwa Naibu Waziri wa Michezo wakati wa Serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
  Bendera ambaye Mei 30, mwaka huu amefikisha umri wa miaka 67, umaarufu wake ulianzia kama kocha wa mpira wa miguu na alikuwa kocha wa timu ya taifa iliyofanikiwa kuitoa Zambia mwaka 1979 na kukata ya Fainali za AFCON mwaka 1980 nchini Nigeria.
  Buriani Joel Nkaya Bendera, kocha aliyeipeleka Tanzania Nigeria mwaka 1980

  Bendera akaendelea kuwa kocha miaka ya 1980 kabla ya kustaafu na kuhamia kwenye siasa ambako alianzia kwa kugombea ubunge wa jimbo la Korogwe mkoani Tanga mwaka 1995 na akafanikiwa kushinda.
  Bendera alilishikilia jimbo hilo hadi mwaka 2010 alipoangushwa kwenye kura za maoni za CCM na Abdallah Nassir Yussuf kwa tofauti ya kura 255 tu.  
  Akiwa Mbunge wa Korogwe, Bendera pia alikuwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo tangu mwaka 2006 hadi 2010. Na ni kipindi hicho ambacho Tanzania ilipata tiketi ya kucheza Fainali za michuano mingine mikubwa Afrika, CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast, michuano inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
  Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Manyara, ambao umekuwa kituo chake cha mwisho cha utumishi wa umma kabla ya kukutwa na umauti. 
  Bendera alikuwa mpenzi wa michezo enzi za uhai zake hususan soka – na aliendelea kujihusisha na mchezo hadi siku za mwisho za uhai wake, akishiriki kuhamaisha michezo kwa watoto.
  Taifa limempoteza mtu muhimu katika sekta ya michezo. Ni pengo ambalo haliwezi kuzibika milele. Anaondoka na rekodi yake pekee ya kukumbukwa milele. 
  Mwalimu pekee aliyeweesha Taifa Stars kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
  Taifa limempoteza mtu muhimu katika sekta ya michezo. Ni pengo ambalo haliwezi kuzibika milele. Anaondoka na rekodi yake pekee ya kukumbukwa milele. Mwalimu pekee aliyeweesha Taifa Stars kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.  
  Mungu ampumzishe kwa amani Mwalimu Joel Nkaya Bendera. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JOEL BENDERA AFARIKI DUNIA LEO MUHIMBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top