• HABARI MPYA

  Sunday, December 03, 2017

  CHALLENGE 2017; KILI STARS YAANZA SHUGHULI NA LIBYA MACHAKOS LEO MECHI LIVE AZAM SPORTS 2

  Na Mwandishi Wetu, MACHAKOS
  MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Challenge Cup, inatarajiwa kuanza leo mjini Nairobi, Kenya hadi Desemba 17, mwaka huu ikishirikisha timu tisa.
  CECAFA ni Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati na lina wanachama 12, na katika kuongeza nakshi katika mashindano yake limekuwa likialika nchi ambazo si wanachama na mwaka huu Libya imekuja kuongeza ushindani.
  Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya, wakati Kundi B lina timu za Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.

  Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya leo Saa 10:00 jioni Uwanja wa Machakos, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda Uwanja wa Kakamega kuanzia Saa 8:00 mchana na mechi zote zitakuwa ‘Live’ chaneli ya Azam Sports 2 ya Azam TV.
  Kili Stars itarudi uwanjani Desemba 7 kumenyana na Zanzibar Heroes, Desemba 9 na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya Desemba 11.
  Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Desemba 12 na Nusu Fainali zitachezwa Desemba 14 na 15, wakati Desemba 17 zitachezwa mechi za kusaka mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali.
  CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
  Wadhamini tofauti wamekuwa wakiingia na kutoka kwa kipindi chote hicho, lakini taarifa zinasema kuanzia mwaka huu Televisheni namba moja Afrika Mashariki na Kati, Azam TV ndiyo wanakuwa wadhamini wapya ambao pia watakuwa wanarusha moja kwa moja michuano hiyo. 
  Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
  Uganda, The Cranes pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 2015 nchini Ethiopia wakiwafunga Rwanda 1-0 kwenye fainali mjini Addis Ababa, wakati mwaka jana michuano hiyo haikufanyika kwa sababu ya kukosa nchi mwenyeji.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHALLENGE 2017; KILI STARS YAANZA SHUGHULI NA LIBYA MACHAKOS LEO MECHI LIVE AZAM SPORTS 2 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top