• HABARI MPYA

  Sunday, December 03, 2017

  ASANTE AZAM TV KUTUREJESHEA CHALLENGE YETU

  MICHUANO ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama CECAFA Challenge Cup, inatarajiwa kuanza leo mjini Nairobi, Kenya hadi Desemba 17, mwaka huu ikishirikisha timu tisa.
  CECAFA ni Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati na lina wanachama 12, na katika kuongeza nakshi katika mashindano yake limekuwa likialika nchi ambazo si wanachama na mwaka huu zinakuja Libya na Zimbabwe kuongeza ushindani.
  Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya, wakati Kundi B lina timu za Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.
  Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.
  Kili Stars itarudi uwanjani Desemba 7 kumenyana na Zanzibar Heroes, Desemba 9  na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya Desemba 11.
  Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Desemba 12 na Nusu Fainali zitachezwa Desemba 14 na 15, wakati Desemba 16 itachezwa mechi ya kusaka mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali.
  CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
  Wadhamini tofauti wamekuwa wakiingia na kutoka kwa kipindi chote hicho, lakini taarifa zinasema kuanzia mwaka huu Televisheni namba moja Afrika Mashariki na Kati, Azam TV ndiyo wanakuwa wadhamini wapya ambao pia watakuwa wanarusha moja kwa moja michuano hiyo. 
  Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
  Uganda, The Cranes pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 2015 nchini Ethiopia wakiwafunga Rwanda 1-0 kwenye fainali mjini Addis Ababa, wakati mwaka jana michuano hiyo haikufanyika kwa sababu ya kukosa nchi mwenyeji.  
  Japokuwa ukanda wa CECAFA ndiyo eneo linalojikongoja kwa sasa katika soka ya kimataifa, lakini ukweli ni kwamba, mpira wa miguu barani Afrika, ulianzia ukanda wa Afrika Mashariki.
  Michuano ya kwanza kabisa mikubwa barani Afrika, ilihusisha mataifa manne, Kenya, Uganda, Tanganyika (sasa Tanzania Bara) na Zanzibar, ikijulikana kwa jina la Kombe la Gossage.
  Michuano hiyo ya Gossage ambayo sasa imekuwa Kombe la Challenge, ilifanyika mara 37 kuanzia mwaka 1926 hadi 1966, ilipobadilishwa jana na kuwa michuano ya wakubwa ya soka kwa mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, ilifanyika mara saba kati ya mwaka 1965 na 1971, ilipozaliwa rasmi CECAFA Challenge.
  Tanganyika ilianza kushiriki michuano hiyo tangu mwaka 1945, wakati Zanzibar ilijitosa miaka minne baadaye, 1949.
  Michuano hiyo ilikuwa ikidhaminiwa na bepari aliyekuwa akimiliki kiwanda cha sabuni, William Gossage, aliyezaliwa Mei 12 mwaka 1799 na kufariki dunia Aprili 9, mwaka 1877.
  Michuano hiyo mikongwe zaidi barani, imekuwa ikiandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ikihusisha timu za taifa za ukanda huo.
  Hadi inafikia tamati michuano ya Gossage, Uganda ilikuwa inaongoza kwa kutwaa taji hilo, mara 22, ikifuatiwa na Kenya iliyotwaa mara 12 na Tanzania mara tano.
  Challenge imetoa wachezaji wakubwa waliocheza Ulaya kama marehemu Majid Musisi wa Uganda, Kalusha Bwalya enzi hizo Zambia haijajitoa CECAFA, Dennis Oliech na wengine kadhaa.    
  Katika orodha hiyo huwezi kuacha kuwataja ndugu Kitwana, Sunday na Kassim Manara waliowahi kuchezea klabu maarufu Tanzania, Yanga.
  Sunday Manara pia alichezea klabu za Almero ya Uholanzi, Odense ya Denmark, Metz ya Ufaransa, Heracles FC Uholanzi, New York Eagles ya Marekani, St. Veit FC ya Austria na Al-Nasri FC ya Dubai alikomaliza soka yake kuanzia mwaka 1981 hadi 1984.
  Kassim Manara alifikia kucheza hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya, akiwa na klabu ya Klangefurt ya Austria. Baadaye Kassim alikwenda Italia, ambako aliitwa na klabu moja huko, lakini hakuna aliyefanikiwa kuelewa mwisho wake ni nini huko. Tangu aondoke, Kassim hajawahi kurudi Tanzania na kwa sasa anaishi Antwerp, Ubelgiji.
  Oliech alitoa mchango mkubwa kwa Kenya kutwaa ubingwa wa Challenge mwaka 2002 mjini Mwanza baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Francis Chinjili na kuifungia Harambee Stars bao la ushindi dakika ya 72 katika fainali ya michuano hiyo Desemba 14, wakiwachapa 3-2 wenyeji Tanzania Bara Uwanja wa Kirumba.
  Siku hiyo, Emmanuel Gabriel alitangulia kuifungia Kilimanjaro Stars katika dakika ya 28, lakini dakika mbili baadaye Paul Oyuga akaisawazishia Harambee Stars, kabla ya Mecky Mexime kuifungia Tanzania Bara bao lililoelekea kuwa la ushindi kwa mkwaju wa penalti dakika ya 59.
  Lakini wakati mamia ya mashabiki wa Kili Stars waliokuwa wamefurika kwenye majukwaa ya CCM Kirumba wanashangilia ushindi, mshambuliaji aliyecheza kwa muda mrefu katika ubora wa hali ya juu kama Rogger Milla wa Cameroon au Madaraka Suleiman wa Tanzania; John Baraza alimtungua kipa chipukizi Juma Kaseja dakika ya 70 na kuisawazishia Kenya bao.
  Bao hilo liliwachanganya wachezaji wa Stars, akina Kaseja, Mexime, Alphonce Modest, Victor Costa, Boniface Pawasa, Suleiman Matola, Ulimboka Mwakigwe, Salvatory Edward, Athumani Machuppa, Emmanuel Gabriel aliyempisha Zubery Katwila dakika ya 74 na Abdul Mtiro aliyempisha Joseph Mwanakusha dakika ya 69, hivyo kuipa nafasi Kenya kuuteka mchezo.
  Hatimaye Oliech wakati huo akiwa anaichezea Harambee Stars akitokea klabu ya Mathare United ya nyumbani kwao, akamtungua Kaseja na kuzima kabisa matumaini ya Watanzania kushangilia taji la tatu la Challenge.
  Kikosi cha Harambee siku hiyo kiliundwa na; Victor Onyango, Adam Shaban, Daniel Agina, George Waweru, Phillip Opiyo, Robert Mambo, Anthony Mathenge, Edward Karanja, Titus Mulama aliyempisha Geoffrey Mangenge ‘Osama’, Francis Chinjili aliyemuachia Oliech, Paul Oyuga aliyempisha Baraza.
  Oliech ndiye alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo kwa mabao yake matano na hata huo ukawa mwanzo wa safari yake ya Ulaya.
  Baada ya kung’ara kwenye michuano hiyo alichukuliwa na Al Arabi ya Qatar aliyoichezea kuanzia 2003 hadi 2005 kabla ya kuhamia Nantes ya Ufaransa, ambayo ilimuuza Auxerre ambako alicheza hadi mwaka huu alipohamia Ajaccio ya huko huko.
  Tangu hapo Challenge imeendelea kuzalisha nyota wengine waliopiga hatua zaidi za kimafanikio kisoka, wakiwemo washambuliaji Mbwana Samatta wa Tanzania na Faruku Miya wa Uganda ambao sasa wanacheza Ubelgiji.
  Wakati Samatta anamaliza mwaka wa pili klabu ya KRC Genk tangu ajiunge nayo kutoka TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Miya anacheza kwa mkopo Royal Excel Mouscron kutoka Standard Liege iliyomtoa Vipers S.C. ya kwao mwaka jana. 
  Samatta anakumbukwa zaidi kwa Challenge ya mwaka 2013 nchini Kenya, ambako aliisaidia Tanzania Bara kufika Nusu Fainali, kabla ya kutolewa kwa mbinde na wenyeji, Kenya kwa kufungwa 1-0 Uwanja wa Nyayo Jijini Nairobi, bao pekee la Alan Wanga wakati huo akitokea El Merreikh ya Sudan.
  Katika michuano hiyo ambayo Samatta alifunga mabao mawili sawa na Mrisho Ngassa, Kili Stars ilikwenda Nusu Fainali kwa kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Uganda kwa kuwachapa kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90. 
  Miya alifanya vizuri zaidi katika fainali za mwaka 2015 nchini Ethiopia akifunga mabao matatu na kuisaidia The Cranes kutwaa Kombe, ikiwafunga Rwanda 1-0 katika fainli.
  Na baada ya kuzikosa fainali hizo mwaka jana kutokana na sababu zilziokuwa nje ya CECAFA, hatimaye Challenge inarejea tena mwaka huu kwa hisani kubwa ya Azam TV. Hii ndiyo Challenge, michuano mikongwe zaidi barani Afrika. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ASANTE AZAM TV KUTUREJESHEA CHALLENGE YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top