• HABARI MPYA

    Sunday, November 19, 2017

    YANGA YAANZA FUJO…YAITANDIKA MBEYA CITY 5-0, CHIRWA APIGA ‘HAT - TRIC’

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imeendelea kula sahani moja na mahasimu Simba katika mbio za ubingwa, baada ya ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 20, sasa inazidiwa pointi mbili vinara Simba SC na Azam FC baada ya timu zote za Dar es Salaam kucheza mechi 10 za Ligi Kuu msimu huu. 
    Shujaa wa ushindi wa Yanga leo ni mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyefunga mabao matatu peke yake, wakati mabao mengine mawili yalifungwa na chipukizi Emmanuel Martin.
    Obrey Chirwa akiinua mikono kuwapigia makofi mashabiki wa Yanga baada ya kufunga mabao matatu leo
    Emmanuel Martin akimuacha chini beki wa Mbeya City, Hassan Mwasapili
    Emanuel Martin (kushoto) akishangilia na Gardiel Michael baada ya kufunga bao la tano
    Hassan Mwasapili akimdhibiti Obrey Chirwa leo Uwanja wa Uhuru 
    Beki chipukizi wa Yanga, Gardiel Michael (kulia) akimiliki mpira dhidi ya kiungo wa Mbeya City, Mrisho Ngassa

    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Athuman Lazi wa Morogoro aliyesaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Abdallah Uhako wa Arusha, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
    Chirwa aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 19 akimalizia pasi ya kiungo Pius Buswita baada ya mabeki wa Mbeya City kuzubaa wakidhani mpira umetoka. 
    Sifa zimuendee Buswita aliyefanya maamuzi ya haraka kwa kumpasia Chirwa aliyekuwa kwenye nafasi nzuri na kufunga.
    Mbeya City walifungwa bao hilo wakitoka kupoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya kiungo wake mshambuliaji, Mrisho Ngassa kupiga shuti jepesi lililodakwa kiulaini na kipa wa Yanga, Mcameroon, Youthe Rostand.
    Emanuel Martin akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 22 baada ya kumlamba chenga kipa wa Mbeya City, Fikirini Bakari kufuatia pasi ndefu ya kutanguliziwa na Buswita.
    Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kutumia vizuri nafasi zao na kujiongezea mabao matatu akianza Chirwa kufunga kwa penalti dakika ya 49 baada ya kiungo Raphael Daudi kuangushwa na kipa kipa Bakari kwenye boksi.
    Mshambuliaji wa zamani wa FC Platinums ya Zimbabwe, Chirwa akakamilisha hat trick yake dakika ya 59 kwa kufunga kiufundi ‘akiuchopu’ mpira juu kuupitisha juu ya kipa mfupi wa Mbeya City na kudondokea nyavuni baada ya pasi ya Ibrahim Ajib na kuamsha shangwe za mashabiki wa Yanga kwa bao hilo la nne.
    Martin akafunga hesabu za mabao ya Yanga leo baada ya kufunga la tano dakika ya 80 akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Gardiel Michael.
    Yanga ingeweza kupata mabao sita kama si winga Geoffrey Mwashiuya kupiga fyongo dakika ya 82 akiwa kwenye boksi na mpira ukaenda nje.
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Pato Ngonyani, Pius Buswita/ Juma Mahadhi dk83, Raphael Daudi, Obrey Chirwa/ Yusuph Mhilu dk75, Ibrahim Ajib/Geoffrey Mwashiuya dk60 na Emmanuel Martin.
    Mbeya City; Fikirini Bakari, Rajab Isihaka, Hassan Mwasapili, Ally Lundenga/Ramadhan Malima dk52, Sankani Mkandawile, Babu Ally, Mrisho Ngassa/Victor Hangaya dk68, Mohammed Samatta, Omary Ramadhani, Frank Ikobela na Eliud Ambokile/Idd Suleiman dk46.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAANZA FUJO…YAITANDIKA MBEYA CITY 5-0, CHIRWA APIGA ‘HAT - TRIC’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top