• HABARI MPYA

  Monday, November 20, 2017

  YANGA SC: TIMU SASA INAANZA KUFUNGUKA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  KOCHA Msaidizi wa Yanga, Nsajigwa Shadrack amesema kwamba ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya Mbeya City unaashiria timu yao inaanza kufunguka sasa.
  Yanga ilishinda 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, Mzambia Obrey Chirwa akifunga mabao matatu na mzawa, Emmanuel Martin akifunga mawili. 
  Na baada ya ushindi huo, Nsajigwa akasema kwamba  wanashukuru kwa kupata pointi tatu muhimu, kwani malengo yao yalikuwa ni kushinda na inapendeza wamepata ushindi mnono.
  “Mwanzoni timu ilikuwa haipati ushindi wa mabao mengi, lakini kwa sasa kikosi chetu kinaanza kufunguka na kupata ushindi mzuri. Ni matarajio yetu tutaendelea hivi hivi, kwa sababu lengo letu ni kutetea ubingwa,”alisema Nsajigwa.  
  Emmanuel Martin (kushoto) akishangilia na Gardiel Michael baada ya kufunga bao la tano
  Ushindi wa jana unaifanya Yanga ifikishe pointi 20, sasa inazidiwa pointi mbili vinara Simba SC na Azam FC baada ya timu zote za Dar es Salaam kucheza mechi 10 za Ligi Kuu msimu huu. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Athuman Lazi wa Morogoro aliyesaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Abdallah Uhako wa Arusha, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
  Chirwa aliifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 19 akimalizia pasi ya kiungo Pius Buswita baada ya mabeki wa Mbeya City kuzubaa wakidhani mpira umetoka, kabla ya Martin kufungia bao la pili dakika ya 22 akimlamba chenga kipa wa Mbeya City, Fikirini Bakari kufuatia pasi ndefu ya kutanguliziwa na Buswita.
  Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kutumia vizuri nafasi zao na kujiongezea mabao matatu akianza Chirwa kufunga kwa penalti dakika ya 49 baada ya kiungo Raphael Daudi kuangushwa na kipa kipa Bakari kwenye boksi.
  Mshambuliaji wa zamani wa FC Platinums ya Zimbabwe, Chirwa akakamilisha hat trick yake dakika ya 59 kwa kufunga kiufundi ‘akiuchopu’ mpira juu kuupitisha juu ya kipa mfupi wa Mbeya City na kudondokea nyavuni kuamsha shangwe za mashabiki wa Yanga kwa bao hilo la nne.
  Martin akafunga hesabu za mabao ya Yanga leo baada ya kufunga la tano dakika ya 80 akimalizia krosi ya beki wa kushoto, Gardiel Michael.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC: TIMU SASA INAANZA KUFUNGUKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top