• HABARI MPYA

  Sunday, November 19, 2017

  TFF IMETUMIA NGUVU NYINGI KUKANUSHA BILA KUJIBU TUHUMA ZINAZOTAJWA KWENYE WARAKA

  UONGOZI mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umetiwa majaribuni baada ya waraka wa tuhuma za ufisadi dhidi yao kusambazwa wiki hii kwenye mitandao ya kijamii.
  Kama ulivyo, bila kuhaririwa waraka huo unasema; “KAMATI TENDAJI YA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF) KUTUMIA MILIONI 438 KWA MWAKA  KUJILIPA POSHO.
  Tarehe 28/10/2017 Kamati ya Utendaji ya TFF, ilifanya Kikao katika Hoteli ya SEA SCAPE Kunduchi Beach jijiji Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine ilipitisha azimio la Wajumbe wa Kamati hiyo kuanza kulipwa posho  ya kila mwezi kwa mchanganuo ufuatao: 
  1. Rais wa  TFF  Tsh.Mil.6 kwa mwezi  sawa na Mil.72 kwa Mwaka.
  2. Makamu wa Rais wa TFF, Tsh. mil. 5  kwa mwezi sawa na Mil.60 kwa mwaka.
  3. Wajumbe 20 wa Kamati ya Utendaji kila mmoja Tsh. Mil. 1 kwa mwezi sawa na mil.12 kwa mwaka ,  kwa wajumbe 20 ni Tsh.  Mil. 240 kwa mwaka.
  NB: Posho hizi ni mpya na hazijawahi kuwepo katika shirikisho hilo katika uongozi uliopita.  
  Aidha Posho za kila kikao zimepanda kutoka Tsh. 300, 000/=  uongozi uliopita hadi laki tano (500,000/) uongozi wa sasa kwa kila mjumbe,  kwa mwaka kuna vikao vya kawaida visivyopungua sita,  kwa Wajumbe wote 22 kwa mwaka itakuwa mil.66. 
  Kwa  mchanganuo huo, Gharama za Posho tu kwa mwaka kwa Wajumbe wa  Kamati ya Utendaji tu ni milioni mia nne thelathini na nane (mil.438). Bado posho za vikao vya dharura, posho za watumishi wengine n.k
  Moja ya changamoto za maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania ni Ukosefu wa fedha.  Timu zetu za taifa zinashindwa kukaa kambini,  Waamuzi wanakosa Mafunzo, viwanja vya michezo vinashindwa kuboreshwa, vilabu vya michezo havisaidiwi na mambo mengine chungu nzima hayafanyiki sababu ya ukosefu wa fedha, leo hii EXCOM  inakwenda kujifungia Sea ESCAPE na kuidhinisha  mil. 438 kwa ajili kujilipa posho!  Kwa mwendo huu tusitegemee maendeleo katika soka Tanzania. Rais wa TFF,  WALES KARIA na Makamu wake, MICHAEL WAMBURA wanapaswa kujitathmini upya,”.
  Baada ya kuzagaa kwa waraka huo, TFF ikaitisha mkutano na Waandishi wa Habari ili kutoa ufafanuzi.
  Na katika mkutano wake na Waandishi wa Habari wiki hii, Kaimu Katibu wa TFF, Wilfred Kidao alionyesha kukasirishwa na waraka huo na akasema shirikisho litawafungulia mashataka watu waliosambaza ujumbe, ambao sio wa kweli.
  Kidau akasema wamekwishapata majina ya watu 10 yanayosambaza ujumbe huo na wanaendelea kuwafuatilia na wengine na baada ya hapo watawafungulia mashitaka hayo, kwani kwa sasa wanazo baadhi ya namba na watazichapisha.
  Tuhuma hizi zinakuja wakati ambao tayari wananchi wamekwishaanza kupoteza imani na viongozi wa michezo wa nchi hii, kufuatia viongozi wengine wa klabu na TFF kukabiliwa na kesi za aina hiyo.
  Ikumbukwe uongozi wa sasa chini ya Rais Wallace Karia na Makamu wake, Michael Wambura uliingia madarakani Agosti 12 mwaka huu katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma, ambao Rais aliyemaliza muda wake, Jamal Malinzi alishindwa kutetea nafasi yake.
  Malinzi alishindwa kutetea nafasi yake kutokana na kuwa rumande akikabiliwa na mashitaka 25, yakiwamo ya utakatishaji fedha wa Dola za Marekani, 375,418 yanayomkabili.
  Malinzi, aliyeingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani – pamoja na aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29, mwaka huu baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya shirikisho hilo iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
  Kwa upande mwingine, viongozi wakuu wa Simba SC, Rais Evans Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakatishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wapo rumande gereza la Keko tangu Juni 29.
  Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya  Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha  likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.
  Kwa sasa nafasi zao zinakaimiwa na Salim Abdallah ‘Try Again’ katika Urais na Iddi Kajuna katika Makamu wa Rais, ambao wamejitahidi kuiongoza vizuri klabu tangu wenzao wapate matatizo hayo.
  Kwa hali kama hii, wazi wananchi na hata vyombo vya dola vitakuwa vimepoteza imani na viongozi wa michezo wa nchi hii, hivyo TFF ilipaswa kuchukua hatua zaidi ya iliyoichukua juu ya waraka huo.
  Kabla ya kufikiria kuwachukulia hatua wanaousambaza waraka huo, TFF ilipaswa kutuaminisha kwamba hizo ni taarifa za uongo.
  Waraka umezama ndani kana kwamba kuna mtu miongoni mwao (TFF) ameuvujisha ukisema hadi vikao vilivyofanyika na vilifanyiwa wapi. Tulitarajia Kaimu Katibu Mkuu angekuwea muwazi zaidi katika mkutano wake, akiuzungumzia kwa undani bila jazba taarifa hiyo.
  Vinginevyo, watu tu watabaki wanajiuliza kwa nini TFF wametumia nguvu nyingi kukanusha na matangazo ya moja kwa moja ya Televisheni na Instagram bila kujibu tuhuma zinazotajwa kwenye waraka wenyewe?   
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF IMETUMIA NGUVU NYINGI KUKANUSHA BILA KUJIBU TUHUMA ZINAZOTAJWA KWENYE WARAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top