• HABARI MPYA

    Tuesday, November 14, 2017

    TAMBWE AANZA MDOGO MDOGO YANGA, MALARIA YAMLAZA TSHISHIMBI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKATI mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe amefanya mazoezi mepesi leo, kiungo Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi hakutokea kabisa.
    Yanga SC imefanya mazoezi leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City Jumapili.
    Tambwe ambaye hajacheza kabisa msimu huu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, alikuwepo leo na kufanya maozezi ya kukimbia pole pole na kunyoosha viungo.
    Majeruhi mwenzake, kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko hakuwepo kabisa, sawa na wachezaji wote waliokuwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars nchini Benin.
    Amissi Tambwe akifanya mazoezi mepesi leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam
    Tshishimbi naye hakuwepo leo na Daktari wa timu, Edward Bavu akasema kwamba mchezaji huyo wa zamani wa Mbabane Swallows ya Swaziland anasumbuliwa na homa ya Malaria.
    Bavu alisema Tshishimbi anaweza kurudi mazoezini kesho sambamba na wachezaji waliokuwa na Taifa Stars nchini Benin.   
    Taifa Stars imerejea nchini alfajiri ya leo kutoka Benin ambako Jumapili ilitoa sare ya 1-1 na wenyeji katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou ambao ulionyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walitangulia kwa bao la la penalti ya utata ya Nahodha wao, Stephane Sessegnon kipindi cha kwanza, kabla ya Elias Maguli kuisawazishia Stars kipindi cha pili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAMBWE AANZA MDOGO MDOGO YANGA, MALARIA YAMLAZA TSHISHIMBI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top