• HABARI MPYA

    Friday, November 17, 2017

    SINGIDA UNITED YAILIPUA LIPULI NA KUJIVUTA JUU LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Singida United imepanda kwa nafasi moja hadi ya tano baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli ya Iringa kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Namfua, Singida.
    Ushindi huo, unaifanya timu ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ifikishe pointi 17 baada ya kucheza mechi 10 na kuishusha Prisons nafasi ya sita. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na Jonesia Rukyaa wa Kagera aliyesaidiwa na Lulu Mushi wa Dar es Salaam na Geoffrey Msakila wa Geita, bao pekee la Singida lilifungwa na nyota wa Rwanda, Danny Usengimana dakika ya 82 akimalizia krosi ya Salum Chuku kutoka upande wa kushoto.
    Prisons wanaweza kurudi juu ya Singida kesho iwapo watashinda dhidi ya Simba SC kesho Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mechi nyingine za kesho Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Stand United na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Maji Maji na Mbao FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mzunguko wa 10 utakamilishwa kwa michezo miwili, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, Yanga watakuwa wenyeji wa Mbeya City na Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, wenyeji Njombe Mji FC wataikaribisha Azam FC.
    Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 19, sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 17, sawa na Mtibwa Sugar.
    Kikosi cha Singida United kilikuwa; Peter Manyika, Michel Rusheshangoga, Shafiq Batambuze, Elisha Moroiwa, Jume Kennedy, Mudathir Yahya, Michael Katsavairo/Elinyesia Sumbi, Tafadzwa Kutinyu, Nhivi Simbarashe/Atupele Green, Danny Usengimana na Kiggi Makasi/Salum Chukwu.
    Lipuli FC; Agathony Anthony, Samuel Mathayo, Ally Sonso, Joseph Owino, Asante Kwesi, Fred Tangalu, Salum Machaku/Seif Abdallah, Mussa Nampaka, Waziri Ramadhani, Malimi Busungu na Shaaban Ada.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SINGIDA UNITED YAILIPUA LIPULI NA KUJIVUTA JUU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top