• HABARI MPYA

  Saturday, November 18, 2017

  SIMBA SC YAICHAPA 1-0 PRISONS NA KUJITANUA KILELENI LIGI KUU

  Na David Nyembe, MBEYA
  SIMBA SC imeanza kuvuta kasi kuelekea kwenye ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Tamu ya ushindi wa Simba leo ni mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 84, baada ya kuwazidi nguvu na maarifa mabeki wa Tanzania Prisons kwenye boksi na kugeuka na kupiga shuti la kiufundi lililomshinda mlinda mlango chipukizi, Aaron Kalambo.
  Kwa ushindi huo, timu ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog inafikisha pointi 22 baada ya kucheza mechi 10 na kuwaacha kwa pointi tatu Azam FC katika nafasi ya pili.
  John Bocco ‘Adebayor’ amefunga bao pekee dakika za lala salama Simba ikiilaza 1-0 Tanzania Prisons 


  Simba iliuanza vizuri mchezo huo na dakika ya 33, winga wake, Shiza Ramadhani Kichuya alipoteza nafasi ya wazi kabisa baada ya kuchelewa kufanya maamuzi akiwa ndani ya boksi kufuatia pasi ya kiungo Haruna Niyonzima na mpira huo kuchukuliwa na na walinzi wa Prisons
  Dakika ya 44 Kichuya tena nusura awainue vitini mashabiki wa Simba kama si shuti lake kwenda nje na dakika ya 45, kipa wa Wekundu wa Msimbazi, Aishi Salum Manula akafanya kazi nzuri kwa kuokoa shuti la Lambert Sibiyanga.
  Kipindi cha pili, Simba walikianza vyema tena na dakika ya 65 Bocco aliunganishia nje kwa kichwa krosi ya Mohammed Ibrahim ‘Mo’.
  Prisons wakajibu dakika ya 72 baada ya mshambuliaji wake, Mohammed Rashid kupiga shuti dhaifu liliookolewa na Manula.
  Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu kabla ya Bocco kuihakikishia SImba pointi tatu dakika ya 84. Huo unakuwa ushindi wa pili mfululizo kwa SImba Jijini Mbeya, baada ya wiki mbili zlizopita kuifunga na Mbeya City 1-0. 
  Mechi za nyingine za Ligi Kuu leo, Ruvu Shooting imeshinda 1-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani, Pwani, Maji Maji imeilaza Mbao FC 2-1 Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Stand United imelazimishwa sare ya 0-0 na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Ikumbukwe hapo jana, Singida United walishinda 1-0 dhidi ya Lipuli FC Uwanja wa Namfua mjini Singida na mzunguko wa 10 utakamilishwa kwa michezo miwili kesho, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, Yanga watakuwa wenyeji wa Mbeya City na Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, wenyeji Njombe Mji FC wataikaribisha Azam FC.
  Kikosi cha Tanzania Prisons kilikuwa; Aaron Kalambo, Michael Ismail, Laurian Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya, Kassim Hamisi, Elivter Mpepo, Mohammed Rashid na Lambert Sibiyanga.
  Simba SC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussen ‘Tshabalala’, James Kotei, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Ally Shomary dk77, John Bocco, Mwinyi Kazimoto/Laudit Mavugo dk66 na Haruna Niyonzima/Mohammed Ibrahim ‘Mo’ dk60.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAICHAPA 1-0 PRISONS NA KUJITANUA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top