• HABARI MPYA

    Thursday, November 16, 2017

    SIMBA SC WAAHIDI KUWAADHIBU PRISONS JUMAMOSI SOKOINE

    Na David Nyembe,  MBEYA
    SIMBA SC imeahidi ushindi dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mratibu wa Simba SC, Abbas Suleiman ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini hapa kwamba kikosi kinaendelea vizuri na maandalizi yake mjini hapa na lengo ni ushindi dhidi ya Prisons.
    Abbas amesema baada ya wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichotoa sare ya 1-1 na wenyeji Benin mjini Cotonou Jumapili kuwasili Jumanne, maandalizi yamepamba moto.
    Amesema wachezaji wana ari kubwa kuelekea mchezo huo na lengo ni kuendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu baada ya ushindi wa 1-0 katika mchezo wao wa kwanza mjini Mbeya wiki mbili zilizopita dhidi ya Mbeya City.
    Amesema timu haina majeruhi mpya, ukiondoa wale watatu wa muda mrefu ambao ni kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na mabeki Shomari Kapombe na Salim Mbonde.    
    Kwa ujumla baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia, Ligi Kuu inatarajiwa kurejea kesho kwa mchezo mmoja tu, Singida United wakiikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Namfua.
    Mechi nyingine za Jumamosi, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Stand United n Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Maji Maji na Mbao FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Mzunguko wa 10 utakamilishwa kwa michezo miwili, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, Yanga watakuwa wenyeji wa Mbeya City na Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, wenyeji Njombe Mji FC wataikaribisha Azam FC.
    Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 19, sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 17, sawa na Mtibwa Sugar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAAHIDI KUWAADHIBU PRISONS JUMAMOSI SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top