• HABARI MPYA

  Saturday, November 18, 2017

  NINJE AMTEMA MSUVA KIKOSI CHA CHALLENGE, AMCHUKUA LYANGA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  KOCHA Ammy Ninje hajamjumuisha winga Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco katika kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge kuanzia Desemba 3, mwaka huu Jijini Nairobi, Kenya.
  Badala yake, Ninje amemchukua winga wa Fanja ya Oman, Daniel Lyanga kwenye kikosi chake cha wachezaji 20 aliowataja leo mjini Dar es Salaam.
  Katika kikosi hicho, Ninje mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ameita makipa wawili tu, Aishi Manula wa Simba na Peter Manyika wa Singida United.  
  Mabeki ni Boniphace Maganga, Gardiel Michael, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Kennedy Wilson.
  Simon Msuva hayumo kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki Kombe la CECAFA Challenge 

  Viungo ni Himid Mao, Hamisi Abdallah, Muzamil Yassin, Raphael Daudi, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Ibrahim Ajib na Abdul Hilal, wakati washambuliaji ni Elias Maguri, Mbaraka Yusuph, Yohana Nkomola na Daniel Lyanga.
  Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya, wakati Kundi B lina timu za Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.
  Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.
  Kili Stars itarudi uwanjani Desemba 7 kumenyana na Zanzibar Heroes, Desemba 9  na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya Desemba 11.
  Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Desemba 12 na Nusu Fainali zitachezwa Desemba 14 na 15, wakati Desemba 16 itachezwa mechi ya kusaka mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali.
  CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
  Wadhamini tofauti wamekuwa wakiingia na kutoka kwa kipindi chote hicho, lakini taarifa zinasema kuanzia mwaka huu Televisheni namba moja Afrika Mashariki na Kati, Azam TV ndiyo wanakuwa wadhamini wapya ambao pia watakuwa wanarusha moja kwa moja michuano hiyo. 
  Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
  Uganda, The Cranes pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 2015 nchini Ethiopia wakiwafunga Rwanda 1-0 kwenye fainali mjini Addis Ababa, wakati mwaka jana michuano hiyo haikufanyika kwa sababu ya kukosa nchi mwenyeji.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NINJE AMTEMA MSUVA KIKOSI CHA CHALLENGE, AMCHUKUA LYANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top