• HABARI MPYA

  Friday, November 17, 2017

  MWANASHERIA AIONYA TFF KUTOIITA TIMU YA TAIFA KILIMANJARO, WATAPOTEZA UDHAMINI WA SERENGETI

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  MWANASHERIA Emmanuel Muga amelionya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuotiita timu ya taifa, Kilimanjaro Stars, kwani kufanya hivyo ni kinyume cha mkataba wa udhamini wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
  Muga alikuwa Mwanasheria wa TFF wakati inasaini mkataba wa udhamini na SBL kwa ajili ya timu ya taifa Mei 12, mwaka huu katika hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam. 
  Na leo Muga amesema; “Mimi ndiye niliyeshughulikia na kusaini mkataba wa kuidhamini timu ya taifa. Sharti moja kuu ni kwamba, timu isiitwe tena Kilimanjaro Stars. Wanaona kama ni kuendelea kuwapa thamani Kilimanjaro (Bia), wadhamini wa zamani. Msikiuke mkataba, msiite Taifa Stars Kili Stars, hata iweje,”.
  Emmanuel Muga (kulia) akishuhudia Rais wa TFF wakati huo, Jamal Malinzi  (wa pili kulia) akitiliana saini na Mkurugenzi wa SBL, Mholanzi, Mama Helene Weesie mbele ya Waziri wa Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe (katikati)

  Mei 12, SBL iliingia mkataba wa udhamini wa Sh. Bilioni 2.1 kwa miaka mitatu na TFF juu ya Taifa Stars katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Kivukoni 4, hoteli ya Serena, Dar es Salaam, hiyo ikiwa mara ya pili kwao, baada ya awali kuidhamini timu hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2008 hadi 2011.
  Katika mkataba huo, SBL iliwakilishwa na Mkurugenzi wae Mkuu, Mholanzi Mama Helene Weesie na TFF iliwakilishwa na Rais wake wa wakati huo, Jamal Malinzi.
  Juhudi za haraka za Bin Zubeiry Sports – Online kumpata Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau kulizungumzia hilo hazikufanikiwa na hata Msemaji, Alfred Lucas hakupatikana pia.
  Lakini inafahamika Taifa Stars ni timu ya taifa ya muungano inayohusisha na wachezaji wa Zanzibar pia, wakati timu ya Bara imekuwa ikijulikana kwa jina la Kilimanjaro Stars na Zanzibar kuna Zanzibar Heroes ambazo zote zimepangwa kundi moja katika michuano ya CECAFA Challenge mwaka huu nchini Kenya.   
  Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya.
  Katika droo iliyopangwa jana mjini Nairobi, Kenya ambako michuano hiyo inafanyika kuanzia Desemba 3 hadi 17, mwaka huu, Kundi B lina timu za Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.
  Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.
  Bado haifahamiki kama TFF itazuia matumizi ya jina Kilimanjaro Stars au, itarudi mezani kwa mazungumzo na wadhamini.
  Wakati huo huo: Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Amy Ninje aliyewahi kucheza Uingereza ameteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars.
  Kwa miezi miwili, Ninje amekuwa mmoja wa Wasaidizi wa Kocha Salum Mayanga Taifa Stars.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWANASHERIA AIONYA TFF KUTOIITA TIMU YA TAIFA KILIMANJARO, WATAPOTEZA UDHAMINI WA SERENGETI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top