• HABARI MPYA

  Wednesday, November 15, 2017

  MBEYA CITY ILIYOIPANIA YANGA YATOA SARE NA COASTAL 2-2 MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  TIMU ya Mbeya City jioni ya leo imelazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji, Coastal Union katika mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
  Coastal walitangulia kupata bao dakika ya sita, kabla ya Omar Ramadhani kuifungia Mbeya City mabao mfululizo dakika za 68 na 78.
  Hata hivyo zikiwa zimesalia dakika sita mchezo kumalizika, Wagosi wa Kaya ambao wanapambana katika Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara kujaribu kurejea Ligi Kuu, wakapata bao la kusawazisha dakika ya 84.
  Mbeya City watawasili Dar es Salaam Ijumaa kutoka Tanga ambako wameweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga


  Meneja wa Mbeya City, Geoffrey Katepa amesema kwamba katika kujiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wameamua kuweka kambi Tanga ambako walifika jana.
  Katepa amesema kwamba wataendelea na mazoezi hadi Ijumaa watakapoondoka mjini Tanga kwenda Dar es Salaam.
  Mbeya City watakuwa wageni wa Yanga Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam Jumapili.
  Na Katepa amesema baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo, wakifungwa 1-0 na zote Azam Dar es Salaam na Simba mjini Mbeya, hawataki kupoteza mechi ya Jumapili.
  “Haitakuwa vizuri tukipoteza na mechi ya Jumapili pia, kwa sababu itakuwa mechi ya tatu mfululizo, ndiyo maana tumeweka program nzuri ya maandalizi tufanye vizuri kwenye mchezo wetu ujao,”amesema Katepa ambaye ni kiungo wa zamani wa Yanga. 
  Kwa ujumla baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia, Ligi Kuu inatarajiwa kurejea wikiendi hii na Ijumaa Singida United wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Namfua, wakati Azam FC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Jumamosi Uwanja wa Saba Saba.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY ILIYOIPANIA YANGA YATOA SARE NA COASTAL 2-2 MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top