• HABARI MPYA

  Sunday, November 12, 2017

  MAGULI AISAWAZISHIA TAIFA STARS YAPATA SARE 1-1 NA BENIN

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou ambao ulionyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa dakika ya 33 kwa penalti na mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Nahodha, Stephane Sessegnon anayechezea klabu ya Montpellier ya Ufaransa.
  Elias Maguri ameonyesha umuhimu wake Taifa Stars akifunga bao la kusawazisha katika sare ya 1-1 na Benin


  Hata hivyo, ilikuwa ni penalti ya mashaka, kwani mchezaji aliyeugusa mpira huo kwa mkono alikuwa ni wa Benin, Khaled Adenon lakini refa akadhani ni mchezaji wa Tanzania.
  Sessegnon akamtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula kufunga bao lake la 21 timu ya taifa katika mechi ya 68.
  Wachezaji wa Tanzania wakamlalamikia refa kwa kutowapa penalti dakika ya 32 kufuatia, winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi baada ya kusukumwa.
  Kipindi cha pili, Tanzania ilikianza kwa nguvu na kasi zaidi wakishambulia kutokea pembeni na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.
  Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Simba ya Tanzania na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri aliyefunga bao hilo akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto dakika ya 50.
  Kiungo wa Tanzania, Mudathir Yahya akatoka anachechemea baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Nurdin Issa Chona dk92. 
  Matokeo haya yanamaanisha Benin imeshindwa kulipa kwa Tanzania, kwani mara ya mwisho, zilipokutana Oktoba 12, mwaka 2014 Taifa Stars ilishinda 4-1, mabao ya Nahodha wa wakati huo, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16, kiungo Amri Kiemba dakika ya 39, Thomas Ulimwengu dakika ya 49 na Juma Luizio, wakati la Benin lilifungwa na Suanon Fadel dakika ya 90.
  Kikosi cha Benin kilikuwa; Fabien Farnole, Rodrigue Fassinou, Khaled Adenon, Cedric Hountonji, David Kiki, Djiman Koukou, Olivier Verdon, Jodel Dossou, Stephane Sessegnon, David Djigla Dossou na Steve Mounie.  
  Tanzania; Aishi Manula, Himid Mao, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Hamisi Abdallah/Jonas Mkude dk75, Simon Msuva/Boniphace Maganga dk85, Mudathir Yahya/Nurdin Chona dk92, Elias Maguli, Raphael Daudi/Mbaraka Yusuph dk54 na Shizza Kichuya/Ibrahim Ajib dk65.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAGULI AISAWAZISHIA TAIFA STARS YAPATA SARE 1-1 NA BENIN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top